Declan Rice ndo jembe lao Arsenal
Muktasari:
- Kwenye uamuzi huo, Arteta alitua Pauni 55 milioni kunasa saini ya Martin Zubimendi, aje kucheza kiungo ya chini, ili Rice asimame juu yake na kufanya vitu vya maana, jambo ambalo limetiki kimtindo.
LONDON, ENGLAND: HABARI ndo hiyo. Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta aliingia sokoni kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi kunasa kiungo wa chini ili kumfanya Declan Rice aanze kuonyesha mavitu yake uwanjani.
Kwenye uamuzi huo, Arteta alitua Pauni 55 milioni kunasa saini ya Martin Zubimendi, aje kucheza kiungo ya chini, ili Rice asimame juu yake na kufanya vitu vya maana, jambo ambalo limetiki kimtindo.
Ujio wa Zubimendi umemfanya Rice kuwa huru na kupunguziwa majukumu ya kukaba. Mashabiki wa Arsenal hivi karibuni walipiga kura kumchagua mchezaji bora wa Arsenal kwa mwaka 2025, ambapo staa Rice ameibuka mshindi.
Kiungo huyo aliyenaswa kwa ada ya Pauni 105 milioni alikuwa mmoja wa wachezaji watano wa Arsenal waliowekwa kwenye mchakato huo wa kupigiwa kura wakati msimu wa 2025/26 ukifika nusu.
Rice ameshindanishwa na mabeki wa kati wawili, Gabriel na William Saliba, kipa David Raya na winga Bukayo Saka. Na Rice aliwaacha mbali wapinzani wake, akipata karibu robo tatu ya kura zilizopigwa.
Kiungo Rice amekuwa mchezaji mwenye msaada mkubwa kwenye kikosi cha Arsenal, ambapo wikiendi iliyopita kwenye mechi ya Ligi Kuu England, kocha Mikel Arteta alifunguka akisema haikumpa shida wakati alipomtaka staa huyo kucheza nafasi ya beki ya kulia baada ya kukosekana mchezaji wa kucheza eneo hilo kutokana na wote kuwa majeruhi.
“Declan ni wa aina yake, anacheza kila eneo, kiongozi ndani ya uwanja na namna anavyopora mipira, hilo linatupa nafasi kubwa sisi kwenda kushambulia,” amesema Arteta.
Kocha wa Everton, David Moyes aliwahi kukiri kuwa Rice ni mmoja wa viungo bora kabisa duniani kwa sasa.