Real Madrid yatuma watu Italia

Muktasari:
- Awali iliripotiwa Madrid inataka kumsajili staa huyu kwa sababu haina uhakika juu ya Vinicius ambaye kuna uwezekano akaondoka mwisho wa msimu huu kutokana na ofa nono aliyowekewa na matajiri wa Saudi Arabia ambao wamekuwa wakimwinda tangu mwaka jana.
MILAN, ITALIA: RIPOTI kutoka Italia zinaeleza, Real Madrid imetuma wawakilishi wake kwenda Italia kwa kukutana na mabosi wa AC Milan na kuanza mazungumzo ya kumsajili winga wao Rafael Leao, 25, dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Awali iliripotiwa Madrid inataka kumsajili staa huyu kwa sababu haina uhakika juu ya Vinicius ambaye kuna uwezekano akaondoka mwisho wa msimu huu kutokana na ofa nono aliyowekewa na matajiri wa Saudi Arabia ambao wamekuwa wakimwinda tangu mwaka jana.
Licha ya Vinicius kuweka wazi angependa kuendelea kusalia Madrid kwa sababu anajisiki furaha kuwa hapo, mabosi wa timu hiyo wana wasiwasi anaweza kubadilisha maamuzi yake, hivyo wamejipanga mapema kuhakikisha wanakuwa na mbadala hilo litakapotokea.
Moja ya sababu zinazoonyesha staa huyu anaweza kuondoka ni mkataba wake ambao unamalizika mwaka 2027 na hadi sasa hajafanya makubaliano ya kuuongeza.
Leao ambaye msimu huu amefunga mabao 10 na kutoa asisti tisa katika mechi 43 za michuano yote, anadaiwa kuwa Madrid ni moja kati ya timu za ndoto zake na angependa siku moja kuichezea.
Hijajulikana ni kwa kiasi gani Milan itakubali kumwachia fundi huyu ingawa taarifa za ndani zinaeleza anaweza kugharimu zaidi ya Pauni 50 milioni.