Real Madrid yatua kwa Ibrahima Konate wa Liverpool

Muktasari:
- Konate ambaye ana mkataba na Liverpool hadi mwaka 2026, ni miongoni mwa mastaa wanaofuatiliwa sana na Madrid ambayo mara kadhaa imekuwa ikituma wawakilishi wake kwenda kumtazama akicheza mechi mbalimbali England.
MABOSI wa Real Madrid wanavutiwa na beki wa Liverpool raia wa Ufaransa, Ibrahima Konate, 25, na inafikiria kumsajili mwisho wa msimu huu ili kuweka sawa eneo lao la ulinzi.
Konate ambaye ana mkataba na Liverpool hadi mwaka 2026, ni miongoni mwa mastaa wanaofuatiliwa sana na Madrid ambayo mara kadhaa imekuwa ikituma wawakilishi wake kwenda kumtazama akicheza mechi mbalimbali England.
Beki huyu anakuwa ni mchezaji wa pili kutoka Liverpool kuhusishwa na Madrid dirisha lijalo, wa kwanza akiwa ni Trent Alexander Arnold.
Tangu kuanza kwa msimu huu Konate amecheza mechi 31 za michuano yote, akifunga mabao mawili na kutoa asisti mbili.
Liverpool huenda ikashawishika kumuuza staa huyu kwa sababu ya mkataba wake kuelekea ukingoni.
Milos Kerkez
LIVERPOOL inataka kutoa Pauni 40 milioni kwenda Bournemouth ili kuipata saini ya beki wa kushoto wa Hungary na Bournemouth, Milos Kerkez, 21, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Kerkez ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028, ni mmoja wa mastaa tegemeo wa Bournemouth ambayo inadaiwa kuhitaji zaidi ya Pauni 50 milioni ili kumuuza.
Angel Gomes
WEST Ham wapo kwenye mazungumzo na wawakilishi wa kiungo wa Lille raia wa England, Angel Gomes, 24, ili kumsajili katika dirisha la majira ya kiangazi huu na atakuwa mchezaji huru baada ya mkataba wake kumalizika. Gomes inadaiwa anataka kuondoka Lille na kutafuta changamoto mpya sehemu nyingine licha ya timu hiyo kumpa ofa ya mkataba mpya.
James Trafford
MANCHESTER United imewaweka katika rada makipa wawili ambao ni James Trafford, 22, kutoka Burnley, na kipa namba moja wa Espanyol, Joan Garcia, 23, ambao huenda ikasajili mmoja wao kwa ajili ya kumpa changamoto kipa wao namba moja raia wa Cameroon, Andre Onana anayeonekana kuwa na makosa mengi tangu kuanza kwa msimu huu.
Bruno Guimaraes
BARCELONA inapambana kuhakikisha inazipiku Arsenal na Manchester City katika mchakato wa kuiwania saini ya kiungo wa Newcastle United na timu ya taifa ya Brazil, Bruno Guimaraes, 27, katika dirisha lijalo. Staa huyu amekuwa akihusishwa na timu mbalimbali barani Ulaya tangu mwaka juzi, lakini changamoto kubwa ilikuwa ni kiasi cha pesa ambacho Newcastle inakihitaji ili kumwachia kinachodaiwa kufikia Euro 100 milioni.
Antony
MSHAMBULIAJ wa Manchester United na timu ya taifa ya Brazil, Antony, 25, ameonyesha tamaa ya kutaka kubakia Real Betis dirisha lijalo la majira ya kiangazi baada ya mkataba wake wa mkopo kumalizika. Antony amekuwa na kiwango bora tangu ajiunge na Betis dirisha lililopita na amecheza mechi saba za michuano yote, akifunga mabao matatu na kutoa asisti mbili.
Tammy Abraham
VIGOGO wa West Ham wameuliza kuhusu upatikanaji wa mshambuliaji wa AS Roma, Tammy Abraham mwenye umri wa miaka 27, ambaye kwa sasa yupo kwa mkopo AC Milan. Tammy amekuwa na panda shuka nyingi hivi karibuni na kabla ya kutua Milan dirisha lililopita kulikuwa na tetesi anaweza kurudi England.
Richarlison
Everton inafikiria kutuma ofa kwenda Tottenham ili kuipata saini ya mshambuliaji wao wa zamani kutoka Brazil, Richarlison, 27, ambaye amekuwa hapati nafasi ya kutosha kikosi cha kwanza Spurs na alifikiria kuondoka tangu mwaka jana na alipokea ofa kutoka Saudi Arabia lakini ilishindikana. Mkataba wa Richarlison unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.