Nunez kuipa hasara Liverpool

Muktasari:
- Nunez, mwenye umri wa miaka 26, alianza vyema alipowasili Anfield akitokea Benfica mwaka 2022, lakini hajakidhi matarajio na msimu uliopita alifunga mabao matano pekee Ligi Kuu England na baadaye akaanza kupoteza nafasi kikosini chini ya Kocha Arne Slot hali inayochochea uvumi Liverpool wapo tayari kumwachia mchezaji huyo.
LIVERPOOL, ENGLAND: LIVERPOOL huenda ikapoteza takribani Pauni 15 milioni dirisha hili ikiwa itamuuza mshambuliaji wao wa kimataifa wa Uruguay, Darwin Nunez.
Nunez, mwenye umri wa miaka 26, alianza vyema alipowasili Anfield akitokea Benfica mwaka 2022, lakini hajakidhi matarajio na msimu uliopita alifunga mabao matano pekee Ligi Kuu England na baadaye akaanza kupoteza nafasi kikosini chini ya Kocha Arne Slot hali inayochochea uvumi Liverpool wapo tayari kumwachia mchezaji huyo.
Napoli kutoka Serie A imejitokeza kuhitaji huduma yake dirisha hili lakini ofa wanayopanga kuiweka mezani inaonekana kuwa ndogo.
Ofa hiyo inadaiwa kuwa ni chini ya Pauni 70 milioni ambayo ni pungufu ya Pauni 15 milioni kutoka Pauni 85 milioni ambayo Liverpool iliilipa ili kumnunua akitokea Benfica miaka mitatu iliyopita.
Liverpool ipo tayari kumuuza ikiwa timu inayomhitaji itatoa Pauni 70 milioni lakini Napoli haiko tayari kulipa kiasi hicho ingawa wanamhitaji sana na rais wao, Aurelio De Laurentiis, ndiye anayeongoza mazungumzo binafsi kuhusu usajili huo.
Kama mpango huo utashindikana, Napoli inapanga kuhamia kwa Lorenzo Lucca wa Udinese kama mbadala.
Kwa sasa, Nunez bado ana mkataba wa miaka mitatu kubaki Anfield na mapema mwaka huu, Arne Slot, alilazimika kukanusha uvumi kuwa muda mdogo wa Nunez kucheza msimu uliopita ulitokana na kipengele katika mkataba wake ambacho kingeilazimu Liverpool kuilipa Benfica Pauni 5 milioni ya nyongeza iwapo angefikisha idadi fulani ya mechi.
Slot alisema: “Je, huwa unaamini kila kitu wanachoandika waandishi wa habari kila wakati? hapana, Na mimi pia huwa siamini. Wakati mwingine inafaa kuwaamini, lakini wakati mwingine bora kupuuza. Hili suala ni geni kabisa kwangu. Nimesema mara nyingi kuwa nafanya kazi kwenye timu nzuri sana.”
“Kwa kweli, mkurugenzi wa michezo huhukumiwa kwa wachezaji anaowaleta. Kwangu mimi ni muhimu kuwa na mazingira mazuri ya kazi na ninayo hapa.”
“Jambo la mwisho kabisa ambalo naamini angefanya baada ya kufanya naye kazi kwa miezi 10 ni kuniambia:
“Ukimchezesha, itatugharimu kiasi hiki, lakini hilo suala halipo na hata kama lipo hawezi kuniambia kabisa. Sijui hata kama ni kweli au si kweli, kwa sababu hatuzungumzii mambo hayo. Hajawahi kuingilia uchaguzi wa kikosi.”