Real Madrid yaivunja nguvu Liverpool dili la Endrick
Muktasari:
- Madrid inamwangalia Endrick kama sehemu muhimu ya mipango yao ya muda mrefu, ikiamini ana uwezo wa kuwa nyota mkubwa wa baadaye.
REAL Madrid haipo tayari kusikiliza ofa kwa ajili ya kumuuza mshambuliaji wake raia wa Brazil, Endrick, 19, ambaye kwa sasa yupo kwa mkopo Olympique Lyonnais.
Madrid inamwangalia Endrick kama sehemu muhimu ya mipango yao ya muda mrefu, ikiamini ana uwezo wa kuwa nyota mkubwa wa baadaye.
Mara kadhaa kumewahi kuwa na tetesi klabu kubwa za Ligi Kuu England zimevutiwa sana na kiwango ambacho fundi huyu amekionyesha akiwa na Lyon, hivyo wanahitaji kumsajili.
Miongoni mwa timu zilizodaiwa kuwa hata katika mazungumzo na wawakilishi wake ni pamoja na Liverpool, ambayo inapambana kutafuta mastaa watakaoboresha timu msimu ujao baada ya kutofanya vizuri msimu huu.
Akiwa na Lyon, Endrick ameonyesha kiwango bora akifunga mabao sita na kutoa asisti sita katika mechi 19 za michuano yote.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa tayari kumwachia mashambuliaji wao Gonzalo Garcia, 22, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Wababe hao wa Hispania wapo tayari kumwachia Gonzalo kwa sababu haonekani kuwa na msaada katika timu na muda mwingi amekuwa akisugua benchi.
Lewis Hall
ARSENAL na Chelsea zinaonekana kuwa ndio zinaongoza mbio za kuiwania saini ya beki wa kushoto wa Newcastle United, Lewis Hall, 21, kuelekea dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Hall ameibuka kuwa mmoja kati ya mabeki vijana wanaovutia zaidi kutokana na uwezo wake wa kushambulia kutoka pembeni.
Hata hivyo, Newcastle inadaiwa kuwa haioo tayari kumwachia kirahisi mchezaji huyo, kwani ni sehemu ya mipango yao ya muda mrefu.
Kutokana na hali hiyo, klabu yoyote itakayohitaji huduma yake italazimika kutoa ofa kubwa ili kuwashawishi mabosi wa Newcastle.
Bart Verbruggen
Kipa wa Brighton na timu ya taifa ya Uholanzi, Bart Verbruggen, 23, anaweza kuondoka dirisha la majira ya kiangazi huku klabu nyingi zikionyesha nia ya kumsajili.
Verbruggen ambaye mkataba wake unamalizika mwaka 2028. Amekuwa akihusishwa na vigogo kadhaa ikiwemo Tottenham ambayo inahitaji kusajili kipa atakayeziba pengo la kipa wao namba moja kwa sasa Guglielmo Vicario anayetarajiwa kuondoka mwisho wa msimu huu kwenda Italia.
Inaelezwa Verbruggen anataka kujiunga na timu itakayompa changamoto zaidi na kushinda mataji.
William Gomes
CHELSEA inapanga kuongeza nguvu katika safu yake ya ushambuliaji na miongoni mwa mastaa inaotaka kuwasajili ili kufanikisha hilo ni winga wa FC Porto, William Gomes, 20.
Nyota huyo wa kimataifa wa Brazil anatajwa kuwa miongoni mwa mastaa hatari katika Ligi Kuu Ureno na maskauti wa timu nying kubwa wamekuwa wakimfuatilia tangu kuanza kwa msimu huu.
Umri wake pia ndio umeonekana kuivutia sana Chelsea ambayo kwa sasa ina malengo ya kujenga kikosi chao kupitia wachezaji vijana sana.
Alisson Becker
LIVERPOOL inapanga kutathmini uwezekano wa kumpa mkataba mpya kipa wake wa kimataifa wa Brazil, Alisson Becker, 33, kuelekea msimu ujao.
Licha ya panda shuka nyingi za matokeo na majeraha, Alisson ameendelea kuwa nguzo muhimu ndani ya kikosi cha Liverpool kwa miaka kadhaa.
Benchi la ufundi la majogoo hao linaamini bado anaweza kuwa namba moja. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Georginio Wijnaldum
KIUNGO wa zamani wa Liverpool na Paris Saint-Germain, Georginio Wijnaldum, 35, ana nia ya kurejea Ligi Kuu England msimu ujao.
Mkataba wake na Al-Ettifaq ya Saudi Arabia, unatarajiwa kumalizika dirisha lijalo la majira ya kiangazi, hali inayomfanya kuwa huru kutafuta changamoto mpya.
Wijnaldum ana uzoefu mkubwa wa soka la England baada ya kung’ara akiwa na Liverpool na alichangia mafanikio makubwa ikiwemo ubingwa wa ligi na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Licha ya umri wake, bado klabu kadhaa zinadaiwa kutaka kumsajili.
Lois Openda
JUVENTUS inapanga kumuuza mshambuliaji wake, Lois Openda, 26, ambaye mwisho wa msimu italazimika kumsainisha mkataba wa moja kwa moja baada ya muda wake wa mkopo kumalizika.
Staa huyu kutoka RB Leipzig alijiunga na Juventus kwa mkopo msimu huu na katika mkataba wake kuna kipengele kinachoeleza wababe hao wa Italia watalazimika kumsainisha mkataba wa moja kwa moja baada ya msimu kumalizika.
Hata hivyo, ripoti zinaeleza Juventus hawana mpango wa kumtumia kwa muda mrefu, hivyo watamuuza punde tu itakapomsainisha mkataba wa kudumu.
David Raum
LIVERPOOL na Manchester United zinapigana vikumbo kuiwania saini ya beki wa kushoto na nahodha wa RB Leipzig, David Raum, 27, baada ya kuvutiwa na kiwango chake alichoonyesha msimu huu.
Raum inadaiwa kupendekezwa na maskauti wa timu hizo ambao wamekuwa wakimchunguza kwa muda mrefu. Staa huyu ambaye pia ameitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani mara kadhaa, mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.