Real Madrid vinara, Man United namba nne

MADRID, HISPANIA. REAL Madrid ni wafalme wa Ulaya na hilo halina mjadala kutokana na uthibitisho wa msimamo wa muda wote wa Ligi ya Mabingwa Ulaya unavyosoma. Los Blancos imewaacha mbali sana wapinzani.
Manchester City yawezekana kuwa ni mabingwa watetezi, lakini Real Madrid linapokuja suala la kuwa wababe wa muda wote, taji hilo haliwezi kuwavuka huko kwenye maskani yao ya Bernabeu.
Real Madrid imeshinda ubingwa huo wa Ulaya mara nyingi kuliko timu nyingine yoyote, mara 14 – mara mbili zaidi ya timu zingine. Hiyo ikiwamo kushinda mara nane katika Ligi ya Mabingwa Ulaya ya mtindo mpya ulioanzishwa mwaka 1992.
Mahasimu wao wakuu kwenye La Liga, Barcelona wanawakaribia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya mpya, ambao walishinda mara ya kwanza msimu wa 1991-92 kipindi hicho ilipokuwa ikifahamika kama Kombe la Ulaya, kabla ya kushinda mara nne zaidi mwaka 2006, 2009, 2011 na 2015.
Lakini, hiyo ni nusu tu ya idadi ya Real Madrid ilivyobeba taji la Mabingwa Ulaya Ulaya katika zama hizi mpya.
Kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Real Madrid haijawahi kushindwa kufuzu hatua ya makundi, mara pekee ambayo walishindwa kuingia kwenye hatua ya mtoano ni msimu wa 1996-97, ambako hawakufuzu.
Barcelona wanashika namba tatu kwenye msimamo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ya zama hizi kwa mujibu wa Transfermarkt. Miamba hiyo ya Nou Camp huenda imeshinda ubingwa mara nyingi kuliko Bayern Munich (mara tatu 2001, 2013, 2020) lakini rekodi zao za ushindi kwenye mechi haziwafanyi kuwashinda wakali hao wa Bundesliga, ambao wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa muda wote kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Real Madrid ni watawala, wakivuna karibu pointi 200 zaidi ya Bayern na wamecheza karibu mechi 100 zaidi.
Msimamo huo wa muda wote umeundwa kwa kuzingatia pointi zilizovunwa kwenye mechi ya ushindi, sare au vichapo, ikihusisha pia mechi za mtoano. Mechi zilizoingia kwenye dakika za nyongeza zinahesabika kama sare.
Manchester United inashika namba nne, ikiwaacha mbali sana wapinzani wao wa Ligi Kuu England.
Man United imekuwa haina makali sana kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa miaka ya hivi karibuni, lakini imevuna pointi nyingi kuzizidi Juventus, AC Milan na Liverpool - ambazo zenyewe zimebeba mataji mengi zaidi kuwazidi.
Man City imekuwa tishio miaka ya karibuni, lakini kwenye msimamo wa muda wote, inashika namba 18 na inazidiwa na timu kama Dynamo Kyiv, Ajax, Benfica na FC Porto.
MSIMAMO HUU HAPA
1. Real Madrid – Pointi 933, mechi 475
2. Bayern Munich – Pointi 747, mechi 377
3. Barcelona – Pointi 649, mechi 332
4. Man United – Pointi 524, mechi 284
5. Juventus – Pointi 521, mechi 297
6. AC Milan – Pointi 430, mechi 260
7. Liverpool – Pointi 432, mechi 230
8. Porto – Pointi 406, mechi 258
9. Benfica – Pointi 403, mechi 262
10. Chelsea – Pointi 355, mechi 197
11. Ajax – Pointi 350, mechi 215
12. Inter Milan – Pointi 330, mechi 196
13. Arsenal – Pointi 309, mechi 188
14. Atletico Madrid – Pointi 262, mechi 157
15. Borussia Dortmund – Pointi 261, mechi 165
16. Paris Saint-Germain – Pointi 252, mechi 140
17. Dynamo Kyiv – Pointi 236, mechi 186
18. Man City – Pointi 219, mechi 118
19. Olympique Lyon – Pointi 210, mechi 136
20. PSV Eindhoven – Pointi 208, mechi 164