Real Madrid kumnunua Trent fasta

Muktasari:
- Miamba hiyo ya Hispania ilipoza mpango wa kumchukua Mwingereza huyo baada ya mabosi wa Liverpool kugomea ofa ya Pauni 20 milioni dirisha la Januari.
MADRID, HISPANIA: REAL Madrid ipo tayari kuilipa Liverpool mkwanja kumnasa Trent Alexander-Arnold kabla ya kufanyika kwa michuano ya Kombe la Dunia la Klabu, Juni mwaka huu.
Miamba hiyo ya Hispania ilipoza mpango wa kumchukua Mwingereza huyo baada ya mabosi wa Liverpool kugomea ofa ya Pauni 20 milioni dirisha la Januari.
Alexander-Arnold anaweza kwenda kujiunga na klabu mpya wakati mkataba wake utakapofika tamati Juni 30. Lakini, Real Madrid inamtaka beki huyo wa kulia mwenye umri wa 26, ili akawe sehemu ya kikosi cha kocha Carlo Ancelotti kwenye fainali za Kombe la Dunia kwa Klabu zitakazofanyika Marekani kuanzia Juni 15. Na hilo litahitaji kukubaliana na Liverpool juu ya ada ya mchezaji huyo.
Msimu wa Liverpool unaweza kufika tamati Mei 31 endapo kama itafika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambayo itapigwa Munich, Ujerumani. Mechi ya mwisho kwenye Ligi Kuu England itapigwa Mei 25. Lakini, kuongoza kwa pointi 15 na bado kuna mechi 10 mbele, hilo linaiweka Liverpool kwenye nafasi nzuri ya kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England kabla ya kufika mwisho.
Dirisha la usajili wa majira ya kiangazi litafunguliwa Juni 1, hivyo mchezaji mpya anaweza kuandikishwa kwenye michuano ya Kombe la Dunia la Klabu.
Kikosi cha Los Blancos kitakabiliana na Al-Hilal ya Saudi Arabia kwenye mechi ya kwanza ya hatua ya makundi huko Miami, Juni 18. Na huko Anfield, kocha Arne Slot hapewi matumaini yoyote ya kumshawishi Alexander- Arnold asaini mkataba mpya wa kuendelea kubaki kwenye timu hiyo.