Rayan Cherki afichua usajili wa Chelsea

Muktasari:
- Cherki alifichua kwamba The Blues ikifanikiwa kumnasa winga huyo itakuwa imepata mtu wa maana kutokana na usumbufu wake ndani ya uwanja na hivyo kubadili upepo wote wa ripoti za awali kwamba miamba hiyo ya Stamford Bridge inafikiria kwenda kumsajili mkali wa Manchester United, Alejandro Garnacho.
LONDON, ENGLAND: STAA mpya wa Manchester City, Rayan Cherki amefichua usajili mpya utakaofanywa Chelsea kwenye dirisha hili kwamba watatua Lyon kwenda kunasa huduma ya mchezaji mwenzake wa zamani, Malick Fofana.
Cherki alifichua kwamba The Blues ikifanikiwa kumnasa winga huyo itakuwa imepata mtu wa maana kutokana na usumbufu wake ndani ya uwanja na hivyo kubadili upepo wote wa ripoti za awali kwamba miamba hiyo ya Stamford Bridge inafikiria kwenda kumsajili mkali wa Manchester United, Alejandro Garnacho.
Kocha Enzo Maresca yupo sokoni kusaka mchezaji wa pembeni kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi baada ya Jadon Sancho kurejea Old Trafford kufuatia mkopo wake kufika tamati na hakuna mpango wa kumchukua jumla. Na ripoti za kuanzia Januari zilidai kwamba Chelsea inamtaka Garnacho na ilielezwa mazungumzo yalishaandaliwa kwa ajili ya kupata saini ya Muargentina huyo mwenye umri wa miaka 20.
Lakini, taarifa mpya zinadai Blues ipo kwenye msako wa mawinga wengine na kwenye hilo wanamfukuzia mkali wa Lyon, Fofana kwa mujibu wa mchezaji mwenzake wa zamani, Cherki, aliyenaswa na Man City dirisha hili.
Fofana alitua kwenye Ligue 1 akitokea Gent mwaka jana. Akiwa na miaka 20, amefunga mabao 11 na asisti sita msimu huu na alikuwa kwenye kiwango bora sana kwenye michuano ya Europa League, ambako alifunga mara sita kabla ya timu hiyo kusukumwa nje na Man United.
Staa huyo wa Kibelgiji kiwango chake bora hakiivutii Chelsea tu, bali klabu nyingine pia ikiwamo Liverpool, Man United na Nottingham Forest kwa mujibu wa L’Equipe, licha ya kwamba miamba hiyo ya City Ground inaweza isinase huduma ya mkali huyo anayethaminishwa kuwa na thamani ya Pauni 42.5 milioni.