Rasmus Hojlund, Victor Osimhen mambo yapo hivi

Muktasari:
- Hata hivyo, ripoti zinaeleza kwamba uwezekano wa kuipata saini ya fundi huyu ni mdogo sana kutokana na kiasi cha pesa ambacho Man United inakihitaji ili kumuuza ingawa kuna uwezekano ikatumika njia nyingine kukamilisha hilo.
NAPOLI inataka kujaribu kutuma ofa kwenda Manchester United kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa timu hiyo na Denmark, Rasmus Hojlund katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Hata hivyo, ripoti zinaeleza kwamba uwezekano wa kuipata saini ya fundi huyu ni mdogo sana kutokana na kiasi cha pesa ambacho Man United inakihitaji ili kumuuza ingawa kuna uwezekano ikatumika njia nyingine kukamilisha hilo.
Ripoti kutoka tovuti ya The Mirror, zinadai Man United inaweza ikakubali kumwachia Hojlund kama sehemu ya mabadilishano ili kumpata Victor Osimhen anayecheza kwa mkopo Galatasaray.
Napoli imekuwa ikitaka pesa ndefu kumuuza Osimhen.
Matheus Cunha
ANDREA Berta anayetajwa kuwa ni Mkurugenzi mpya wa michezo wa Arsenal ni shabiki mkubwa wa mshambuliaji wa Wolves na Brazil, Matheus Cunha, 25, ambaye ana kipengele kinachomwezesha kuuzwa mwisho wa msimu huu ikiwa timu inayomhitaji italipa Pauni 62.5 milioni ili kuvunja mkataba wake.
Cunha ambaye msimu huu amefunga mabao 15, amekuwa katika kiwango bora sana akitingisha EPL. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2029.
Eduardo Camavinga
KIUNGO wa Real Madrid na Ufaransa, Eduardo Camavinga, 22, anafikiria kujiunga na Manchester City katika dirisha hili kwa sababu ya kupata nafasi kubwa zaidi ya kucheza jambo ambalo anaona hatolipata akiendelea kusalia Madrid.
Mbali ya Man City, Camavinga pia anawindwa na Chelsea ambayo ipo tayari kufanya mabadilishano ya wachezaji kwa kumtoa Enzo Fernandez kisha yenyewe impate staa huyo wa Ufaransa.
Marco Asensio
KOCHA wa Aston Villa, Unai Emery anapambana kuhakikisha timu hiyo inafanikiwa kumsainisha mkataba wa kudumu mshambuliaji wa Paris St-Germaun na Hispania, Marco Asensio, 29, katika dirisha lijalo mara baada ya mkataba wake wa sasa wa mkopo kumalizika.
Emery anahitaji Asensio asainishwe mkataba mpya kutokana na kiwango bora alichoonyesha tangu ajiunge nao kwa mkopo.
Kobbie Mainoo
MABOSI wa Manchester United wapo tayari kusikiliza ofa kutoka kwa timu mbalimbali zinazohitaji saini ya kiungo wao raia wa England, Kobbie Mainoo, 19, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Kobbie ambaye mkataba wake unamalizika mwaka 2027, ameripotiwa kugoma kusaini mkataba mpya wa kuendelea kusalia kwenye kikosi hicho kwa sababu ya ofa ndogo ambayo amewekewa mezani.
Bernardo Silva
KIUNGO wa Manchester City na Ureno, Bernardo Silva, 30, amepanga kuendelea kusalia kwenye kikosi hicho kwa msimu ujao na kumalizia mkataba wake licha ya ripoti zinazodai kwamba anahitajika na timu za Saudi Arabia.
Silva ambaye kwa sasa yupo nje kutokana na majeraha, msimu huu amecheza mechi 38 na kufunga mabao matatu.
Ansu Fati
BARCELONA ipo tayari kumuuza mshambuliaji wao raia wa Hispania, Ansu Fati katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi licha ya kugoma kuondoka Januari mwaka huu ambapo kulikuwa na timu zaidi ya nne zilizohitaji kuipata huduma yake. Fati mwenye umri wa miaka 22, amekuwa hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza.
Jobe Bellingham
MANCHESTER United ni kati ya timu zinazohitaji saini ya kiungo wa Sunderland na England, Jobe Bellingham,19, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Jobe ambaye ni mdogo wa Jude Bellingham wa Real Madrid, mkataba wake wa sasa na Sunderland unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.