Newcastle United yaingilia dili la Man United kwa Lewin

Muktasari:
- Staa huyu ambaye kwa sasa ni mchezaji huru, hivi karibuni alidaiwa kuwa katika rada za Manchester United ambayo kwa sasa inatafuta sana mshambuliaji.
NEWCASTLE imefanya mazungumzo na straika wa zamani wa Everton, Dominic Calvert-Lewin, 28, ili kumsajili dirisha hili.
Staa huyu ambaye kwa sasa ni mchezaji huru, hivi karibuni alidaiwa kuwa katika rada za Manchester United ambayo kwa sasa inatafuta sana mshambuliaji.
Inadaiwa kocha wa Newcastle Eddie Howe ni shabiki wa muda mrefu wa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa England ambaye aliondoka Everton baada ya mkataba wake kwisha mwezi uliopita.
Hadi sasa bado haijajulikana ni wapi mshambuliaji huyu atatua katika dirisha hili kwani timu zote zinaendelea kufanya mazungumzo na hakuna iliyofikia katika hatua nzuri.
Wilfred Ndidi
KIUNGO wa Leicester City na timu ya taifa ya Nigeria, Wilfred Ndidi, 28, ni miongoni mwa wachezaji ambao wapo katika rada za Manchester United inayohitaji saini yake. Katika mkataba wake Ndidi ana kipengele kinachomwezesha kuachiliwa ikiwa timu inayomhitaji italipa pauni 9 milioni baada ya Leiecester kushuka daraja. Fulham, Everton na Crystal Palace pia zinamnyatia.
Denzel Dumfries
INTER Milan ina wasiwasi huenda Manchester City au Barcelona moja wapo italipa Euro 25 milioni katika dirisha hili kabla ya Juni 15 kwa ajili ya kuipata saini ya beki wao wa kimataifa wa Uholanzi Denzel Dumfries, 29. Katika mkataba wake Dumfries ana kipengele ambacho kinamruhusu kuondoka kabla Julai 15 ikiwa timu atakayokubaliana nayo italipa euro 25 milioni.
Neil El Aynaoui
SUNDERLAND, Leeds United na Wolves zinapambana kumsajili kiungo wa kati wa Lens na timu ya taifa ya Morocco chini ya miaka 23, Neil El Aynaoui, lakini wanakabiliwa na ushindani kutoka AS Roma, Juventus na AC Milan ambazo pia zinahitaji saini ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24. Hata hivyo, ripoti zinadai Neil mwenyewe anatamani sana kwenda kucheza Ligi Kuu England kwa sababu ni ndoto yake.
El Hadji Malick Diouf
KOCHA wa Slavia Prague, Jindrich Trpisovsky, amethibitisha El Hadji Malick Diouf yuko mbioni kuondoka kwenye timu yake dirisha hili jambo linalozidisha tetesi staa huyo ni kweli anaweza kutua England ambako anahusishwa na timu mbalimbali kama West Ham na Leeds United. Beki huyu wa kimataifa wa Senegal ana umri wa miaka 20.
Son Heung-min
TIMU za Saudi Arabia, Al-Ahli, Al-Nassr na Al-Qadsiah zimeonyesha nia ya kumsajili mshambuliaji wa Tottenham Hotspur na Korea Kusini, Son Heung-min, mwenye umri wa miaka 32 na kila timu ipo tayari kutoa Pauni 34 milioni kama ada ya uhamisho. Son ambaye amekataa mara kadhaa ofa ya kujiunga na timu hizo za Saudia, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwakani.
Granit Xhaka
AC Milan imekutana na wawakilishi wa Bayer Leverkusen na kiungo wao wa kimataifa wa Uswizi, Granit Xhaka, mwenye umri wa miaka 32 kwa ajili ya kujadili uwezekano wa kuipata huduma yake dirisha hili. Xhaka inadaiwa kuonyesha nia ya kujiunga na Milan baada ya kupendezwa na mipango yao kuelekea msimu ujao.
Anthony Elanga
WINGA wa Nottingham Forest, Anthony Elanga anatarajiwa kusafiri kwenda Newcastle United kwa ajili ya vipimo vya afya baada ya timu hizo mbili kufikia makubaliano ya mauziano. Kwa mujibu wa Skysports, Nottingham imekubali kumuuza staa huyu wa kimataifa wa Sweden mwenye umri wa miaka 23, kwa Pauni 55 milioni.