Rashford ataka kushinda taji la Ulaya Villa Park
Muktasari:
- Kwenye mahojiano yake ya kwanza tangu alipoachana na Manchester United kwenda kujiunga na Aston Villa kwa mkopo, fowadi huyo wa England alifichua dhamira yake ya kushinda taji kubwa kabisa kwenye ngazi ya klabu.
BIRMINGHAM, ENGLAND. Marcus Rashford ametamba kwamba bado ana uwezo wa kuziadhibu timu hivyo atafanya hivyo kuisaidia Aston Villa kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwenye mahojiano yake ya kwanza tangu alipoachana na Manchester United kwenda kujiunga na Aston Villa kwa mkopo, fowadi huyo wa England alifichua dhamira yake ya kushinda taji kubwa kabisa kwenye ngazi ya klabu.
Rashford atavaa jezi Namba 9 huko Villa Park — ambayo iliachwa wazi na mshambuliaji Jhon Duran, ambaye ametimkia zake Al Nassr kwa dili la Pauni 70 milioni kwenye dirisha la Januari lililofungwa Jumatatu iliyopita.
Rashford alisema: “Kurudi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ni kitu kinachovutia sana. Ni michuano mikubwa kwa klabu kushiriki, hakika zimekuwa zikifanya kuwa na usiku wa aina yake kwenye soka. Tunataka kufika mbali kwa kadri tunavyoweza na kama hatuna dhamira ya kushinda, basi hatuwezi kushinda.
“Nina hakika kitakuwa kitu chenye wigo mkubwa wa uzoefu kwa mimi kuichezea Aston Villa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Najua naweza kuziadhibu timu, ninapokuwa kwenye ubora wangu, nimekuwa na uwezo wa kubadili matokeo kwenye mechi. Hayo yatakuwa malengo yangu kuisaidia timu kushinda mechi nyingi, pointi nyingi na bila shaka tutatengeneza historia.”
Rashford amefunga mabao 12 na kuasisti mara tatu katika mechi 33 alizochezea Man United kwenye michuano ya Ulaya. Na sasa huko Villa Park, Rashford atakwenda kuungana na Marco Asensio, ambaye naye amejiunga na Aston Villa kwa mkopo akitokea Paris Saint-Germain.
Rashford, 27, aliongeza: “Nimecheza mechi nyingi za Ligi ya Mabingwa Ulaya hivyo nadhani nitatumia uzoefu wangu kupambana na mechi za aina hiyo. Itakuwa mara yangu ya kwanza kucheza michuano ya Ulaya nikiwa na timu nyingine, lakini hilo linavutia zaidi kuliko kuogopesha.”
Aston Villa imetinga hatua ya mtoano ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, hivyo kocha Unai Emery ameongeza wachezaji wenye uzoefu wa michuano hiyo kama Rashford na Asensio ili kwenda kufanya vizuri kwenye michuano hiyo.