Rakitic hatamani kucheza na Messi

BARCELONA, HISPANIA. NI wachezaji wachache sana ambao wamewahi kumtolea nje Lionel Messi, na kiungo wa Sevilla, Ivan Rakitic ambaye waliwahi kucheza Barcelona, ameonyesha kutovutiwa na kujiunga na Inter Miami.

Kulikuwa na mapendekezo kwamba mchezaji huyo mkongwe wa kimataifa wa Croatia anaweza kuungana na mchezaji mwenzake wa zamani wa Barcelona huko Marekani.

Messi tayari ameungana na wachezaji wenzake wa Barcelona, Sergio Busquets na Jordi Alba, huku Luis Suarez ikisemekana huenda akaelekea Inter Miami.

Rakitic, ambaye alicheza Camp Nou kwa miaka sita kati ya mwaka 2014 na 2020, amepuuzia mazungumzo kuhusu uwezekano wa kujiunga na Inter Miami pale mkataba wake utakapomalizika Sevilla.

Akijibu ujumbe kwenye mtandao wa kijamii ambao uliuliza swali: “Rakitic kwenda Inter Miami?”, kiungo huyo mwenye umri wa miaka 35 alisema: “Inaweza kutokea, lakini nadhani nitabaki Sevilla, kuna maana kubwa juu ya makubaliano ya mdomo au kusaini mkataba wa miaka miwili. Tuone kitakachotokea.”

Rakitic aliwahi kusema ataongeza mkataba na Sevilla: “Sifikirii juu ya kitu kingine chochote zaidi ya kucheza hapa, kuendelea hapa na Sevilla, hakuna sehemu nzuri zaidi ya Sevilla. Siwezi kusema kama nilizaliwa hapa lakini nitafia hapa.”

Pia kumekuwa na mazungumzo kwamba Rakitic amehusishwa na klabu za Saudi Arabia, lakini staa huyo ameonyesha kufurahia maisha Sevilla na hana mpango wa kuondoka kumfuata Cristiano Ronaldo.