Pyramids yaitibulia Mamelodi, Mayele anusa ubingwa CAFCL

Muktasari:
- Pyramids FC haijawahi kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika na Mamelodi Sundowns imechukua ubingwa huo mara moja ambayo ni 2016
Dar es Salaam. Mamelodi Sundowns imejiweka rehani nafasi ya kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani na Pyramids FC ya Misri jana.
Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Lucas Moripe, Pretoria, Kusini, bao la kuongoza la Mamelodi Sundowns lilipachikwa na Lucas Ribeiro katika dakika ya 54.
Ribeiro alipachika bao hilo akimaliza kwa shuti la mguu wa kushoto mpira uliookolewa na mlinzi wa Pyramids FC baada ya shuti la Aubrey Modiba.
Lakini wakati wengi wakiamini Sundowns inapata ushindi katika mechi hiyo, Walid El Karti aliisawazishia Pyramids FC katika dakika za majeruhi akimalizia kwa kichwa krosi ya Mohanad Lasheen.
Matokeo hayo yanaiweka Pyramids FC katika nafasi nzuri ya kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika kwani inahitaji ushindi wa aina yoyote au sare tasa katika mechi ya marudiano ambayo itakuwa nyumbani, Cairo Misri, Juni Mosi ili itwae ubingwa.
Ikiwa mchezo huo wa marudiano utamalizika kwa sare ya mabao ya kuanzia 2-2 au Pyramids FC kupoteza, Mamelodi Sundowns itatwaa ubingwa na kama utamalizika kwa sare ya bao 1-1, mikwaju ya penalti itatumika kusaka mshindi.
Kama Pyramids FC itatwaa ubingwa, litakuwa taji la kwanza kwake la mashindano ya Klabu Afrika kama ilivyo kwa mshambuliaji wake Fiston Mayele ambaye nusura atwae Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022/2023 alipokuwa na Yanga ambayo ililikosa mbele ya USM Alger ya Algeria baada ya mechi mbili za fainali baina ya timu hizo kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Mchezo wa leo umesisimua wengi ambao wametazama kutokana na timu zote mbili kufunguka mara kwa mara na kushambuliana tangu filimbi ya mwanzo ilipopulizwa hadi dakika 90 zilizpofikia tamati.
Katika mchezo huo, benchi la ufundi la Mamelodi Sundowns lilifanya mabadiliko ya kuwapumzisha Tashreek Matthews, Iqraam Rayners, Arthur Sales na Lucas Ribeiro ambao nafasi zao zilichukuliwa na Peter Shalulile, Neo Maema, Thapelo Morena na Jayden Adams.
Pyramids FC iliwatoa Ahmed Atef, Ibrahim Adel na Fiston Mayele ambao nafasi zao zilichukuliwa na Ramadan Sobhi, Karim Hafez na Marwan Hamdi.