PSG yajitoa kumwania Rashford

MANCHESTER, ENGLAND. SASA ni rasmi mshambuliaji wa Manchester United Marcus Rashford bado yupo yupo sana katika kikosi cha mashetani hao wekundu baada ya ripoti kufichua Paris Saint- Germain  hawana mpango naye.

Rashford, 26, amekuwa akihusishwa na PSG katika siku za hivi karibuni ili akazibe pengo la  Kylian Mbappe anayeondoka mwisho wa msimu huu.

Mkataba wa sasa wa Rashford ambao amesaini katika siku za hivi karibuni na unaomwezesha kukunja Pauni 325,000 unamalizika mwaka 2028.

Chanzo kutoka kwa mtu wa karibu na staa huyu  kimefichua kuhusishwa kwa Rashford na PSG ilikuwa ni kwa sababu ya kumfanya staa huyo apate pesa nyingi katika mkataba wake mpya lakini hakukuwa na ofa yoyote,

“PSG haijawahi kuvutiwa na Marcus, ukizingatia amekuwa kwenye kiwango kibovu ndo hawezi kwenda kabisa, ilikuwa inatumika kama sehemu ya kuboresha maisha yake ndani ya Man United.”

Staa huyu wa kimataifa wa England alikuwa sehemu ya kikosi cha Man United kilichocheza na Bournemouth wikiendi iliyopita na kutoka sare ya mabao 2-2.

Tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 39 za michuano yote, akafunga mabao nane na kutoa asisti tano.

Amekuwa kwenye kesi nyingi sana za nje ya uwanja ikiwa pamoja na kwenda kujirusha klabu na kuacha kwenda mazoezini kosa lililosababishwa atozwe faini ya Pauni 600,000 kabla ya mambo yote kumalizwa na kurejeshwa katika kikosi.

Hii inakuwa ni mara yapili kwa Rashford kuhusishwa na baadhi ya timu kubwa barani Ulaya, msimu wa mwaka juzi Barcelona iliripotiwa kutaka kumsajili lakini hakuna kilichotokea na Rashford akaendelea kuitumikia Man United.