PSG, Barca ni mechi ya kisasi
Muktasari:
- Katika mechi ya robo fainali msimu uliopita, PSG iliitoa Barca kwa matokeo ya jumla ya mabao 6-4 baada ya kuicha mabao 4-1 katika mechi ya mkondo wapili.
BARCELONA, HISPANIA: LIGI ya Mabingwa inaendelea tena kesho lakini macho na masikio yote yatakuwa pale Lluis Companys Olympic Stadium na wenyeji Barcelona watakuwa wanaikaribisha Paris Saint-Germain katika mechi ya kisasi itakayoanza saa 4:00 usiku.
Mechi hii inaonekana kuwa ya kisasi zaidi kwa Barcelona kutokana na mambo mawili ambayo yalitokea msimu uliopita.
Katika mechi ya robo fainali msimu uliopita, PSG iliitoa Barca kwa matokeo ya jumla ya mabao 6-4 baada ya kuicha mabao 4-1 katika mechi ya mkondo wapili.
Mbali ya kisasi hiki cha kutolewa, Barca pia ilipigwa nje ya Uwanja na PSG katika tuzo za Ballon D’or ambapo staa wao Lamine Yamal alikuwa akishindana na fundi Ousmane Dembele wa PSG na matokeo yake Mfaransa huyo akashinda tuzo hiyo.
Yamal ambaye alikuwa na majeraha amerejea na anaweza kupangwa katika mechi hii lakini mpinzani wake katika tuzo hizo hatokuwepo kutokana na majeraha yanayomsumbua.
Rekodi zinaonyesha katika mechi 10 zilizopita ambazo timu hizi zilikutana katika michuano hii, Barcelona imeshinda tano, moja ikamalizika kwa sare kisha PSG ikashinda nne.
Timu zote hizi zilishinda mechi zao za kwanza za mashindano haya na kabla ya mechi za jana PSG ilikuwa ikishika nafasi ya pili kwa pointi zao tatu wakati Barca ikiwa ya 12.
Mbali ya mechi hii, kutakuwa na mechi nyingine nane na Arsenal iliyoshinda mechi yake ya kwanza dhidi ya Athletic Bilbao itakuwa nyumbani kuikaribisha Olympiacos ya Ugiriki.
Man City ambayo msimu huu imeanza kwa panda shuka, imesafiri hadi Ufaransa kuvaana na AS Monaco wakati mabingwa wa msimu uliopita wa Serie A watakuwa nyumbani kwenye Uwanja wao wa Diego Armando Maradona kuikarisha timu ya zamani ya Kocha Ruben Amorim, Sporting Lisbon.
Mechi za mapema kwa kesho ni Qarabag FK dhidi ya Copenhagen na Union Saint-Gilloise dhidi ya Newcastle ambazo zote zitaanza saa 1:49 usiku.