Romário: Nitaipenda Barcelona hadi kufa kwangu
Muktasari:
- Nyota huyo wa zamani wa Brazil, aliitumikia Barcelona katika sehemu ya maisha yake ya soka, ambapo pia alitwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia wa FIFA mwaka 1994.
Gwiji wa Barcelona, Romário de Souza Faria, amefichua kwamba angechagua kuiwakilisha Argentina badala ya kuchezea Real Madrid, jambo linaloonyesha uhusiano wake wa dhati na klabu ya Barcelona ni kama samaki na maji.
Nyota huyo wa zamani wa Brazil, aliitumikia Barcelona katika sehemu ya maisha yake ya soka, ambapo pia alitwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia wa FIFA mwaka 1994.
Romario aliulizwa achague kati ya kuchezea Argentina ambayo ni mshindani mkubwa wa Brazil kisoka, au Real Madrid ambayo ni mpinzani wa Barcelona, lakini gwiji huyo alijibu angechezea Argentina.
“Nitacheza Argentina. Mimi ni wa Barcelona hadi kufa,” amesema kupitia @RoyNemer kwenye X.
Romario alianza kucheza soka akiwa na Vasco Da Gama nchini Brazil kabla ya kuhamia PSV Eindhoven baada ya kushinda kiatu cha dhahabu kwenye Olimpiki za 1988. Alitumia misimu mitano katika klabu hiyo ya Uholanzi, akifunga mabao 165 katika mechi 167 kabla ya kutua Barcelona.
Romario alikaa kwa miaka miwili pekee katika Uwanja wa Nou Camp lakini aliacha alama kubwa, akitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia wa FIFA akiwa na klabu hiyo mwaka 1994.
Anakumbukwa zaidi kwa kufunga hat-trick katika ushindi wa 5-0 kwenye mechi ya El Clasico dhidi ya Real Madrid, Januari 1994. Alifunga mabao matatu na kutoa pasi mbili za mabao katika mechi tano za El Clasico dhidi ya Los Blancos, akishinda mara mbili.
Akiwa mmoja wa wachezaji wakubwa wa enzi zote, Romario alicheza mechi 65 tu ndani ya Barcelona, akifunga mabao 39 na kutoa asisti 17. Licha ya muda mfupi aliotumia katika klabu hiyo, bado anajitambulisha kikamilifu kama ‘Culer’, jambo linaloashiria uhusiano wa kina wa kihisia na Barcelona.