Wachambuzi wampa Dembele Ballon d’Or
Muktasari:
- Sherehe ya Ballon d’Or mwaka huu inatazamiwa kufanyika Jumatatu ijayo, ambapo mastaa wengi wanagombea tuzo hiyo ya heshima.
PARIS, UFARANSA: MALEJENDI Thierry Henry na Jamie Carragher wameweka wazi wachezaji ambao wanawapa nafasi kubwa ya kushinda tuzo ya Ballon d’Or ya mwaka 2025 kuelekea sherehe za tuzo hizo zinazotarajiwa kufanyika wiki ijayo.
Sherehe ya Ballon d’Or mwaka huu inatazamiwa kufanyika Jumatatu ijayo, ambapo mastaa wengi wanagombea tuzo hiyo ya heshima.
Ousmane Dembele, Lamine Yamal, Kylian Mbappe na Mohamed Salah ni miongoni mwa wachezaji wanaotajwa kupewa nafasi kubwa ya kuichukua.
Dembele aliiongoza Paris Saint-Germain kutwaa mataji manne makubwa msimu uliopita, likiwamo la Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku Yamal akionyesha kiwango bora Barcelona na kuisaidia timu ya taifa ya Hispania kushinda Kombe la Euro 2024.
Vilevile Mbappe na Salah walionyesha viwango bora wakiwa na timu zao kiasi cha kupewa nafasi kubwa ya kushinda taji hilo.
Baada ya mechi za Ligi ya Mabingwa Jumatano, zilizoshuhudiwa ushindi kwa Barcelona na Manchester City, Jamie Carragher na Henry walijadili Ballon d’Or kupitia kituo cha televisheni cha CBS Sports.
Mtangazaji Kate Scott, ambaye atakuwa ndio MC wa hafla ya Ballon d’Or, aliibua mjadala kuhusu mbio hizo.
Carragher alitaja majina ya Dembele, Mbappe, Salah, Yamal, Raphinha na Achraf Hakimi kama mastaa anaowapa nafasi kubwa lakini gwiji huyo wa Liverpool alimuunga mkono Dembele kushinda tuzo hiyo kutokana na kiwango chake alichoonyesha akiwa na PSG.
Kwa upande wa Henry, yeye alimtaja Dembele kama ndio mchezaji pekee anayempa nafasi ya kushinda taji hilo, akisisitiza kwamba haitaji hata kuelekeza juu ya hilo.
Mkurugenzi wa michezo wa PSG, Luis Campos, pia amesisitiza kuwa Ousmane Dembele ambaye msimu uliopita alifunga mabao 35 katika michuano yote anastahili kushinda Ballon d’Or.