PSG bado wamtamani Rashford

Muktasari:
- Awali PSG ilijaribu kumsajili staa huyo mwaka 2022, lakini dili likafeli na baadaye ikaelezwa kuwa haikuwa na mpango wa kumchukua wakati huo.
PARIS, UFARANSA: WABABE wa Ufaransa, Paris Saint-Germain wanadaiwa kuwa bado wanaitamani huduma ya mshambuliaji wa Manchester United na timu ya taifa ya England, Marcus Rashford ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo Aston Villa.
Awali PSG ilijaribu kumsajili staa huyo mwaka 2022, lakini dili likafeli na baadaye ikaelezwa kuwa haikuwa na mpango wa kumchukua wakati huo.
Hivi karibuni zimeibuka tena tetesi zikidai PSG inamwangalia Rashford kama mbadala sahihi wa Kylian Mbappe ambaye alitimkia Real Madrid. Wakala wa Rashford na PSG wamekutana zaidi ya mara tatu huko Ufaransa kujadili uwezekano wa staa huyu kujiunga nao tangu mwaka 2022, inaripoti L’Equipe. Rashford kwa sasa anafanya vizuri katika kikosi cha Aston Villa anakocheza kwa mkopo, ikiwa ni baada ya kupitia kipindi kigumu akiwa na Man United.
Jana staa huyu alipata nafasi kucheza na PSG ambapo ripoti zinaeleza ilikuwa ni nafasi nyingine ya PSG kumtazama zaidi staa huyo mwenye umri wa miaka 27 hususani kocha kocha Luis. Kabla ya mchezo wa PSG, Rashford alikuwa amefunga mabao matatu na kutoa asisti nne tangu ajiunge na Villa Januari.