Potter atambulishwa West Ham, afunguka
Muktasari:
- Potter mwenye umri wa miaka 49, anachukua nafasi ya Lopetegui, ambaye alifutwa kazi, Jumatano baada ya kuhudumu kwa miezi sita tu.
LONDON, ENGLAND: BAADA ya kukaa nje ya gemu kwa mwaka mmoja na miezi 10, hatimaye kocha wa zamani wa Chelsea na Brighton, Graham Potter amepata shavu la kuinoa West Ham United akichukua mikoba ya Julien Lopetegui.
Potter mwenye umri wa miaka 49, anachukua nafasi ya Lopetegui, ambaye alifutwa kazi, Jumatano baada ya kuhudumu kwa miezi sita tu.
Inaelezwa, mabosi wa West Ham walishafikia mwafaka wa kumfukuza Lopetegui tangu wiki iliyopita lakini walikuwa wakihitaji kwanza kuandaa mbadala wake.
Inaelezwa walianza mazungumzo na Potter wiki hii kabla ya kufikia makubaliano na kumsainisha mkataba wa miaka miwili na nusu.
Potter ambaye atatakiwa kuirudisha West Ham katika nafasi za juu kutoka ilipo sasa ambapo inashika nafasi ya 14 baada ya kucheza mechi 20, amesema alikaa nje kwa muda mrefu kwa sababu alihitaji ajira inayomfaa zaidi.
“Ninashukuru kuwa hapa. Ilikuwa muhimu kwangu kusubiri hadi kupata nafasi ambayo nilihisi inanifaa na naamini mimi ni mtu sahihi kwa timu hii. Mazungumzo yangu na mwenyekiti na bodi yamekuwa mazuri na yenye kujenga, tunafikiria jambo moja katika kujenga misingi thabiti itakayoweza kuzalisha mafanikio, na tuna mawazo sawa kuhusu kile kinachohitajika kwa muda mfupi na jinsi tunavyotaka kuendeleza timu kwa muda wa kati hadi mrefu,” alisema Potter.
“West Ham United ni klabu kubwa, katikati ya London, na mashabiki wakubwa wanaoipenda timu hii duniani kote. Niliona matukio yaliyoambatana na ushindi wao wa Europa Conference League mwaka 2023 na ilikuwa dhahiri kuwa hii ni klabu kubwa.”
Kocha huyu atakuwepo katika benchi kwa mara ya kwanza leo, Ijumaa pale West Ham itakapoivaa Aston Villa Kombe la FA.
Kabla ya kuteuliwa kwake, Potter alikuwa bila kazi tangu Aprili 2023 alipondoka Chelsea baada ya mfululizo mbaya wa matokeo ikiwa ni baada ya miezi saba tangu kuajiriwa kwake.
Kabla ya kutua Chelsea, Potter alihudumu kwa miaka mitatu akiwa Brighton, pia aliwahi kuzifundisha Swansea, Ostersund na Leeds Carnegie.