Pointi 40 zitatosha? Vita ya kushuka daraja EPL yapamba moto
Muktasari:
- Lakini kinachoulizwa kwa sasa ni je pointi 40 zitatosha kweli kubaki kwenye Ligi Kuu England (EPL)? Baada ya ushindi wa Tottenham Hotspur, West Ham United na Nottingham Forest mwishoni mwa wiki iliyopita, vita ya kushuka daraja imepamba moto. Kuna uwezekano kwamba pointi 40 hazitatosha timu kubaki kwenye Ligi Kuu England.
LONDON, ENGLAND: LIGI Kuu England (EPL), imetinga katika hatua ya 34 ikiwa imebakiza raundi nne ili kumalizika kwa msimu wa 2025/26 unatarajiwa kukamilika ifikapo Mei 24, mwaka huu, lakini ikiwa imejikita sasa katika dakika za mwishomwisho za vita ya kufuzu mashindano ya Ulaya na kushuka daraja, Championship.
Lakini kinachoulizwa kwa sasa ni je pointi 40 zitatosha kweli kubaki kwenye Ligi Kuu England (EPL)? Baada ya ushindi wa Tottenham Hotspur, West Ham United na Nottingham Forest mwishoni mwa wiki iliyopita, vita ya kushuka daraja imepamba moto. Kuna uwezekano kwamba pointi 40 hazitatosha timu kubaki kwenye Ligi Kuu England.
Kwa miaka mingi kuna dhana kwamba timu ikifikisha pointi 40 inakuwa salama zaidi katika msimamo wa ligi hiyo, kwa sasa inaonekana kuwa si sahihi kutokana na jinsi mambo yalivyo. Kwa timu zinazopambana kutoshuka daraja mambo ni magumu hata zikifikia kiwango hicho.
Katika misimu 21 iliyopita ni mara moja ambapo timu iliyomaliza nafasi ya 18 ilifikisha pointi 39 ambayo ni Birmingham City 2010/11.
Hiyo ndiyo mara moja pekee katika zaidi ya miongo miwili ambapo pointi 40 zilihitajika kubaki. Kipindi hicho wastani wa pointi za timu iliyomaliza nafasi ya 18 ni takribani 33.5.
Katika kila msimu kati ya 14 iliyopita, pointi 38 zimetosha kubaki, huku timu zote zilizomaliza nafasi ya 18 zikifikisha kiwango cha juu cha pointi 37 tu na hata hilo lilitokea mara moja tu (Newcastle United msimu wa 2015/16).
Katika misimu ya awali ya EPL yenye mechi 38 (1995 hadi 2003), kulikuwa na matukio matatu ambapo hata pointi 40 hazikutosha kubaki.
Tukio la mwisho lilikuwa 2002/03, ambapo West Ham United walishuka daraja wakiwa na pointi 42. Hata hivyo, licha ya matukio hayo, wastani wa pointi za timu iliyomaliza nafasi ya 18 katika historia ya misimu ya mechi 38 ni takribani 34.5. Hivyo, inaonekana pointi 40 siyo ajabu kuweza kubaki.
Wastani huo pia umeathiriwa na misimu ya hivi karibuni ambapo baadhi ya timu zilishuka daraja zikiwa na pointi chache sana mfano Fulham 2020/21 ((28), Luton Town 2023/24 (26) na Leicester City msimu uliopita (25). Katika misimu hiyo, pointi 40 zilitosha kubaki salama.
Hata hivyo, msimu huu hali ni tofauti. Timu zinazopambana kubaki zinahitaji pointi nyingi zaidi kuliko kawaida. Kutokana na kiwango kizuri cha timu zilizo chini ya msimamo, kuna uwezekano mkubwa kwamba zaidi ya pointi 40 zitahitajika.
West Ham United, Nottingham Forest na Leeds United zote zimepata matokeo mazuri kwa wakati muafaka. Leeds hawajapoteza katika mechi tano, Forest hawajapoteza sita na West Ham wameshinda sita kati ya mechi 13 za mwisho.
Zikiwa zimebaki mechi nne, West Ham wako nafasi ya 17 wakiwa na pointi 36 mbili juu ya mstari wa kushuka daraja. Hii ni tofauti na msimu uliopita ambapo walikuwa na pointi kama hizo lakini walikuwa mbali na hatari hiyo.
Kwa upande wa Spurs wako kwenye nafasi ya kushuka daraja kwa sasa, juu ya timu ambazo tayari zimeshuka kama Burnley na Wolverhampton Wanderers.
Hata hivyo, ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Wolves uliwapa matumaini mapya. Spurs walimaliza msimu uliopita nafasi ya 17 wakiwa na pointi 38, lakini safari hii wanaweza kushuka daraja hata wakifikisha kiwango kikubwa zaidi ya hicho. Kwa sasa wana pointi 34, wakiwa na uwezekano wa kupata hadi pointi 12 kutokana na mechi zilizobaki.
Kwa mujibu wa makadirio ya kompyuta ya Opta, Spurs ndio wana uwezekano mkubwa zaidi wa kushuka daraja (asilimia 59), wakitarajiwa kumaliza na wastani wa pointi 38.7.
Hata hivyo, bado wana nafasi ya kufikisha pointi 40 kama watashinda mechi mbili. Ratiba yao inajumuisha mechi dhidi ya Leeds na Everton nyumbani pamoja na mechi ngumu ugenini dhidi ya Aston Villa na Chelsea.
Kwa upande wa West Ham, wana ratiba ngumu zaidi lakini wako kwenye kiwango kizuri. Wanahitaji ushindi mmoja na sare moja kufikisha pointi 40, jambo linalowezekana kabisa kwa sasa.
Forest wana pointi 39 na wanatarajiwa kufikisha pointi 40 kwa urahisi kutokana na kiwango chao cha hivi karibuni. Leeds tayari wamefika kiwango hicho.
Hii ina maana kwamba timu zote nne zinaweza kufikisha pointi 40 na kwa hiyo, moja bado italazimika kushuka daraja licha ya kufikia “alama ya usalama”.
Ingawa Spurs wako kwenye hali mbaya zaidi wana matumaini baada ya kutopoteza mechi mbili mfululizo kwa mara ya kwanza tangu Februari.
Tatizo ni kwamba wapinzani wao wote wako kwenye kiwango kizuri pia. Ukiangalia mechi tatu za mwisho, timu zote nne ziko katika 10 bora kwa matokeo bora ya hivi karibuni.
Pia kuna uwezekano mdogo kwamba Newcastle United ambao wamekwama kwenye pointi 42 tangu Machi 14, wanaweza kuingia kwenye hatari ya kushuka daraja.
Hata hivyo, bado kuna uwezekano mkubwa kwamba Spurs watapoteza mechi zilizosalia na kuendelea na mwenendo wa kawaida wa timu inayoshika nafasi ya 18 kutofikisha pointi 40.
Kwa ujumla, idadi halisi ya pointi itategemea matokeo ya Spurs na West Ham. Ikiwa wataendelea kushinda, basi timu nyingine zitaingia kwenye hatari zaidi, na huenda msimu huu ukaweka rekodi mpya ya pointi nyingi zaidi kwa timu inayoshuka daraja.
Kwa mara ya kwanza tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000, inawezekana kabisa kwamba pointi 40 hazitatosha kubaki Ligi Kuu England.