Pogba mambo yazidi kwenda mrama
Muktasari:
- Pogba alirejea uwanjani kwa mara ya kwanza Novemba mwaka jana, baada ya kupita zaidi ya miaka miwili tangu alipocheza mechi yake ya mwisho.
MONACO, UFARANSA: MAISHA yamezidi kuwa magumu kwa staa na kiungo wa zamani wa Manchester United, Paul Pogba ambaye, amepata pigo jingine baada ya kuondolewa kwenye kikosi cha Monaco kitakachoshiriki hatua za mtoano za Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Pogba alirejea uwanjani kwa mara ya kwanza Novemba mwaka jana, baada ya kupita zaidi ya miaka miwili tangu alipocheza mechi yake ya mwisho.
Kiungo huyo alijiunga na Monaco kwa uhamisho huru Juni mwaka jana, baada ya kumaliza kutumikia adhabu ya kufungiwa kwa miezi 18 kutokana na matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni.
Licha ya kusajiliwa, Pogba alitakiwa kusubiri kwa muda ili kurudi katika utimamu wa mwili kabla ya kucheza mechi hiyo ya Ligue 1 dhidi ya Rennes aliyoingia akitokea benchini.
Baada ya hapo, Pogba amecheza mechi mbili zaidi akiingia kama mchezaji wa akiba, lakini amekosa mechi tisa zilizopita katika mashindano yote kutokana na majeraha.
Hali hiyo imesababisha aondolewe katika kikosi kitakachoshiriki mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya na inadaiwa kwamba sababu kubwa haijulikani lini atapona jeraha lake.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, kupitia RMCSport, mkurugenzi wa Monaco, Thiago Scuro, amesema: “Idara nzima ya tiba imeweka nguvu zote katika kutafuta suluhisho juu ya jeraha lake. Hakuna jibu la wazi juu ya lini atarudi. Bado tunahitaji kuendeleza mchakato ili kufafanua zaidi.”
Mbali na Pogba, beki Mohammed Salisu na kiungo Takumi Minamino pia wameondolewa kwenye kikosi, huku wote wakikosa mechi kadhaa zilizopita kutokana na majeraha.
Wachezaji waliosajiliwa Januari, Wout Faes na Simon Adingra, wameingia kuchukua nafasi zao, huku Krepin Diatta naye akiongezwa kwenye kikosi.
Monaco itacheza tena Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumanne, Februari 17, itakapokuwa wenyeji wa PSG katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa mchujo.
Mchezo wa mkondo wa pili utafanyika katika uwanja wa Parc des Princes Jumatano, Februari 25 na mshindi wa matokeo ya jumla atakutana na kati ya Barcelona au Chelsea katika hatua ya 16 bora.