Pique kapiga bao la  kujifunga kwa Shakira

BARCELONA, HISPANIA. WANASEMA kama huna wa kukubembeleza, usinune. Supastaa, Gerard Pique anajutia kuachana na mrembo Shakira na alihitaji warudiane mwezi tuu baada ya kupigana vibuti, imeelezwa.

Staa huyo wa zamani wa Barcelona, Pique aliripotiwa kutaka kurudiana na mwimbaji huoyo wa pop, mrembo wa Colombia mwezi tu baada ya kuachana.

Na Shakira aligoma kurudiana na Pique na kumfanya staa huyo kuangukia kwenye penzi la mrembo wa miaka 23, Clara Chia Marti.

Taarifa hizo zimefichuliwa na mwandishi Mhispaniola, Jordi Martin - ambaye alizungumza na mtu wa karibu wa Shakira. Kilichotokea, Pique aliamua kusitisha uhusiano wake na mrembo Shakira, Aprili mwaka jana.

Lakini, mwezi mmoja tu baadaye, baada ya kuondoka nyumbani na kuacha familia yake, alirudi kwa mwimbaji huyo na kumtaka asahau yaliyopita ili warudiane na waishi kama zamani. Martin alisema: "Pique alijutia kuachana na Shakira na alitaka warudiane."

Kwa sasa Pique amenasa kwenye penzi la mwanafunzi wa Uhusiano wa Umma, mrembo Clara Chia Marti.

Mwandishi huyo aliongeza: “Kutoka kwa watu wa karibu wa Shakira, waliniambia wawili hao uhusiano wao ulikufa Aprili mwaka jana. Mwezi mmoja baadaye, Pique alijutia uamuzi na kurudi nyumbani, lakini mambo hayakuwa vizuri, wakaachana moja kwa moja. Kipindi hicho tayari alishakuwa na Clara."

Mwandishi huyo alisema Shakira, ambaye alimsamehe Pique kwa kuchepuka huko nyuma, safari hii hakuwa na uvumilivu huo baada ya kufahamu kwamba kuna mrembo Clara amemkamatia mwanamume huyo.

Na kulipa kisasi, Shakira alitoa wimbo mpya ambao ndani yake kuna mashairi yanatosema: "Sitarudiana na wewe, hata kwa kulia au kunipigia magoti."

Na wimbo huo una kijembe kwa Clara kutokana na umri wake, kupitia shairi linalosema: “Nina thamani ya miaka 22 mara mbili. Umefanya biashara ya kubadili Ferrari kwa Twingo, umebadili Rolex kwa Casio.”

Na Pique katika kujibu mapigo alienda kazini kwake na gari aina ya Renault Twingo yenye thamani ya Pauni 8,000 huku mradi wake wa King’s League ukipata udhamini wa Casio.