Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

PIGWA UTOKE! Mtoano Ligi ya Mabingwa Ulaya moto umeanza kuwaka

Muktasari:

  • Hiyo ni kwenye mtoano wa hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo itashuhudia vipute vya maana, ikiwamo Madrid derby na moto wa Paris Saint-Germain na Liverpool.

MADRID, HISPANIAL: ILE hatua ya ngumi jiwe kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya sasa imefika. Ukipigwa mara ya kwanza, unapewa nafasi ya kujiuliza, ukishindwa tena kupindua mechi, imekula kwako. Unatupwa nje.

Hiyo ni kwenye mtoano wa hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo itashuhudia vipute vya maana, ikiwamo Madrid derby na moto wa Paris Saint-Germain na Liverpool.

Mtoano huo, mechi nne zitapigwa Jumanne na nne nyingine ni Jumatano. Patamu hapo.


Club Brugge vs Aston Villa (Machi 4, saa 2:45 usiku)

Club Brugge haijashinda kwenye mechi 14 za michuano ya Ulaya dhidi ya timu za England kabla ya penalti ya kipindi cha pili ya Hans Vanaken iliyowapa ushindi 1-0 mbele ya Aston Villa kwenye mechi ya nne ya hatua ya makundi. Na sasa miamba hiyo inakutana tena kwenye mtoano wa hatua ya 16 bora na kufanya mechi hiyo kuwa ya timu zinazofahamiana kimtindo. Ikiwa imepata somo kwenye mechi ya kwanza, kocha Unai Emery atakuwa na kibarua cha kuchanga vyema karata zake ili raundi hii, ambayo ukizubaa, unatupwa nje.

Kitu kitamu kuhusu mechi hiyo ni kwamba Club Brugge imewahi kupata ushindi mara saba tu kati ya 30 ilizokutana na rimu za England katika michuano ya UEFA (Sare5,  vichapo 18).


Real Madrid vs Atletico de Madrid (Machi 4, saa 5:00 usiku)

Macho ya wengi yatakuwa kwenye kipute hiki cha mahasimu wa jiji la Madrid, Real Madrid na Atletico Madrid. Mechi hiyo ni kama marudio ya fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya 2014 na 2016, mechi mbili kati ya nne za hatua ya mtoano zilizokutanisha timu hiyo kati ya mwaka 2014 na 2017. Sasa miaka minane, baadaye, miamba hiyo inakutana tena kwenye hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Balaa hilo.

Mechi zao walizokutana kwenye La Liga msimu huu, zilimalizika kwa sare ya 1-1, jambo ambalo litafanya kipute hicho cha mtoano kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kuwa na upinzani zaidi. Uzuri timu hizo zote mbili zina rekodi nzuri ya kushinda dhidi ya wapinzani wa Kihispaniola kwenye michuano ya Uefa. Real Madrid imepoteza mara tano kati ya 23 (imeshinda 12, sare 6), wakati Atleti imegoma kufungwa kwenye mechi 14 kati ya 21 (imeshinda 9, sare 5 na vichapo 7).


PSV vs Arsenal (Machi 4, saa 5:00 usiku)

Bao la ushindi la dakika za majeruhi la Ryan Flamingo lilitosha kuifanya PSV kutinga hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya mbele ya Juventus katika mechi ya mchujo. Wakichagizwa na mzuka huo, miamba hiyo ya soka ya Uholanzi inaamini itafanya kweli kwenye mtoano huo wa hatua ya 16 bora kwa kumenyana na miamba ya soka ya Ligi Kuu England, Arsenal. Mara ya mwisho, timu hizo kukutana kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ilikuwa msimu uliopita, mechi ya kwanza kabisa hatua ya makundi, ambapo Arsenal ilishinda 4-0. Lakini, safari hii, Arsenal itaingia uwanjani bila ya huduma ya mastaa wake muhimu akiwamo Bukayo Saka, Kai Havertz, Gabriel Martinelli na Gabriel Jesus, ambao ni majeruhi. Hiyo itakuwa mara ya 11 kwa timu hizo kukutana kwenye michuano ya Uefa, huku Arsenal ikishinda nne, sare nne na vichapo viwili.


Borussia Dortmund vs Lille (Machi 4, saa 5:00 usiku)

Mabao 10 ya Serhou Guirassy, ikiwamo moja kati ya matatu yaliyoisaidia Dortmund kuitupa nje Sporting CP kwenye mchujo wa kuania kutinga hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya yalimfanya kuingia kwenye msako wa tuzo ya kinara wa mabao. Na sasa, jukumu lake lijalo ni kuhakikisha Dortmund inapenya kwenye 16 bora wakati itakapokabiliana na miamba ya Ufaransa, Lille. Kocha wa Dortmund, Nico Kovac ni mtu mwingine mwenye uzoefu na soka la Ufaransa, aliwahi kuinoa AS Monaco. Guirassy alifunga mfululizo kwenye mechi tano za Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya kutoka suluhu kwenye mechi yao ya pili dhidi ya Sporting CP.


-Feyenoord vs Inter (Machi 5, saa 2:45 usiku)

Robin van Persie atakuwa kocha wa tatu kuiongoza Feyenoord kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, akikabidhiwa mikoba hiyo kwenye hatua hii ya 16 bora baada ya timu huyo kuachana na Brian Priske aliyewaongoza kwenye hatua ya makundi na Pascal Bosschaart kwenye mchujo dhidi ya AC Milan. Feyenoord imerudishwa tena kwa mpinzani kutoka Italia kwenye hatua hii ya mtoano wa 16 bora, mahasimu wa mpinzani wao aliyepita kwenye mchujo. Lakini, Inter ni timu yenye safu ngumu sana ya mabeki, ambapo kwenye hatua ya makundi, timu iliyopata bao mbele yao ilikuwa Bayer Leverkusen tu. Hilo linafanya mechi kuwa tamu.

Kitu unachopaswa kufahamu kuhusu kipute hicho kitamhusu Lautaro Martinez, akiwa mchezaji wa tatu wa Inter aliyeweka rekodi ya kufunga hat-trick kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.


Paris Saint-Germain vs Liverpool (Machi 5, saa 5:00 usiku)

Ushindi wa jumla wa 10-0 dhidi ya Wafaransa wenzao Brest kwenye mechi ya mchujo wa kuingia hatua ya 16 bora umetuma ujumbe mzito kwa wapinzani wanaofuata kwenye njia ya Paris Saint-Germain kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaa msimu huu. Na sasa mpinzani aliyesimama mbele yao ni Liverpool ya supastaa Mohamed Salah. Mechi hiyo inatazamwa kama ni fainali iliyotangulia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, ambapo mashabiki wanatazamia kuona mechi ya upinzani mkali muda wote. PSG inaamini inaweza kufanya jambo baada ya ushindi wao wa mabao 4-2 dhidi ya Manchester City ya Ligi Kuu England kwenye hatua ya makundi, wakati Liverpool yenyewe ilipata ushindi mwembamba mbele ya Lille inayocheza Ligue 1 sambamba na PSG. Patamu hapo. Usichokijua ni kwamba ushindi ule wa 10-0 iliyopata PSG mbele ya Brest ni mkubwa zaidi kwenye tofauti ya mabao kuwahi kutokea kwenye mtoano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.


Bayern Munich vs Leverkusen (Machi 5, saa 5:00 usiku)

Bayern Munich ilibeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mara ya mwisho ilipokutana na timu nyingine ya kutoka Ujerumani kwenye michuano hiyo, iliichapa Dortmund 2-1 kwenye fainali ya 2013 uwanjani Wembley. Lakini, safari hii, Bayern itakumbana na mabingwa wa Bundesliga, Bayer Leverkusen kwenye mtoano wa hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Patachimbika. Leverkusen msimu huu inaburuzwa na Bayern kweye vita yao ya kutetea taji la Bundesliga, lakini kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya huko mambo ni tofauti kabisa. Nani atatoboa? Mechi hiyo itakuwa mtihani mzito kwa straika Harry Kane kuhakikisha anafukuzia ndoto zake za kubeba mataji makubwa, ambayo yamekuwa adimu kwenye soka lake.


Benfica vs Barcelona (Machi 5, saa 5:00 usiku)

Kama matokeo ya timu hizo mbili zilipokutana kwenye hatua ya makundi ni dalili ya kitakachokwenda kutokea kwenye raundi ya 16 bora, basi Barcelona itakwenda kushinda kipute hicho mbele ya miamba hiyo ya Ureno. Barcelona imekuwa na matata sana msimu huu chini ya kocha Hansi Flick, lakini itakwenda kumenyana na Benfica yenye kocha mwenye uzoefu wa aina fulani, Bruno Lage katika mikikimikiki hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambayo ipo kwenye hatua ambayo ukizembea tu unatupwa nje usubiri msimu ujao. Kitu kizuri ni kwamba Barcelona inakutana na timu ambayo yenyewe pia inafahamu namna ya kufunga mabao. Benfica ni moja ya timu mbili ambazo zilifunga mabao manne dhidi ya Barcelona kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.


Utamu zaidi

Mechi za pili za hatua hiyo ya mtoano zitapigwa Jumanne ya Machi 11 na Jumatano ya Machi 12, kufahamu timu nane zitakazotinga robo fainali. Kwenye robo fainali, mechi za kwanza zitakuwa Jumanne, Aprili 8 na Jumatano, Aprili 9, huku zile za marudiano zitafanyika wiki moja inayofuatia. Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu huu, itapigwa Mechi 31 huko uwanjani The Munich Football Arena.