Georgina Rodriguez avunja ukimya
Muktasari:
- Safari ya Ronaldo katika Kombe la Dunia ilihitimishwa kwa maumivu baada ya Ureno kuchapwa bao 1-0 na Hispania kwenye mchezo uliopigwa Dallas, huku bao la dakika za majeruhi lililofungwa na Mikel Merino likimaliza rasmi ndoto zake za kutwaa taji hilo kubwa zaidi la soka duniani.
ATLANTA, MAREKANI:MCHUMBA wa nahodha wa Ureno, Cristiano Ronaldo, Georgina Rodriguez, amevunja ukimya kwa kumuonyesha sapoti nyota huyo baada ya ndoto yake ya kutwaa Kombe la Dunia kufikia mwisho.
Safari ya Ronaldo katika Kombe la Dunia ilihitimishwa kwa maumivu baada ya Ureno kuchapwa bao 1-0 na Hispania kwenye mchezo uliopigwa Dallas, huku bao la dakika za majeruhi lililofungwa na Mikel Merino likimaliza rasmi ndoto zake za kutwaa taji hilo kubwa zaidi la soka duniani.
Ronaldo, mwenye umri wa miaka 41 na mchezaji pekee aliyefunga mabao katika Kombe la Dunia mara sita tofauti, alionekana akitoka uwanjani akiwa analia baada ya kipyenga cha mwisho, ishara ya mwisho wa safari yake ya kihistoria akiwa na timu ya taifa ya Ureno.
Baada ya kipigo hicho, Georgina Rodriguez alituma ujumbe mfupi lakini wenye uzito kupitia ukurasa wake wa Instagram. Mrembo huyo mwenye wafuasi zaidi ya milioni 74.7 alishiriki upya chapisho la kampuni ya Nike, mdhamini wa muda mrefu wa Ronaldo, lililokuwa na picha ya mshambuliaji huyo pamoja na maneno: "His Legend Lives On", kisha akaambatanisha emoji ya moyo mwekundu kuonyesha upendo na kumuunga mkono.
Kabla ya mashindano hayo kumalizika, Ronaldo alikuwa amethibitisha kuwa Kombe la Dunia la mwaka huu nchini Marekani, Canada na Mexico lingekuwa la mwisho kwake, ingawa alitamani mchezo dhidi ya Hispania usingekuwa wa mwisho katika historia yake ya michuano hiyo.
Baada ya Ureno kuondolewa, nyota huyo alisisitiza uamuzi wake wa kustaafu Kombe la Dunia akisema:
"Ndiyo, hili limekuwa Kombe langu la Dunia la mwisho. Sasa nitapata muda wa kufikiria, kuwa na familia yangu na maisha yanaendelea."
Licha ya kushindwa kutwaa Kombe la Dunia, Ronaldo amesema hana majuto kwa kile alichokifanya akiwa na timu ya taifa.
"Nitaamka kesho nikiwa na dhamira safi kwa sababu nilitoa kila kitu. Nimeipa Ureno mataji matatu, wakati kabla yangu haikuwa imewahi kushinda chochote. Kwangu, ubingwa wa Euro 2016 una thamani sawa na Kombe la Dunia," amesema.
Katika maisha yake ya kimataifa, Ronaldo aliiongoza Ureno kutwaa ubingwa wa Euro 2016 pamoja na mataji mawili ya UEFA Nations League mwaka 2019 na 2025.
Baada ya mahojiano ya mwisho uwanjani, Ronaldo alielekea vyumbani akiwa amevunjika moyo, huku picha zake akilia zikikumbusha tukio la mwaka 2022 nchini Qatar, alipoondolewa na Morocco katika robo fainali ya Kombe la Dunia na kuonekana akilia alipokuwa akielekea vyumbani.