Piga ua, Arsenal lazima isajili

Muktasari:
- Baada ya kusumbuliwa sana na majeruhi msimu huu na kisha kutokuwa na idadi kubwa ya wachezaji, jambo hilo limewapa somo Arsenal na bila shaka hawatataka ijurudie msimu ujao.
LONDON, ENGLAND: BILA kujali itamalizaje msimu wa 2024-25, Arsenal itahitaji kufanya usajili wa kuboresha kikosi chao dirisha lijalo.
Baada ya kusumbuliwa sana na majeruhi msimu huu na kisha kutokuwa na idadi kubwa ya wachezaji, jambo hilo limewapa somo Arsenal na bila shaka hawatataka ijurudie msimu ujao.
Bado kuna muda wa kutosha wa kikosi hicho cha Mikel Arteta kumaliza msimu kikiwa matawi ya juu, wakati sasa kikiwa nyuma kwa pointi 12 dhidi ya vinara wa Ligi Kuu England, Liverpool, lakini bado wapo kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kwenye hatua ya robo fainali watakipiga na Real Madrid.
Kama itavuka kwenye kizingiti cha Real Madrid itakwenda kukutana na ama Paris Saint-Germain au Aston Villa kwenye nusu fainali. Haijawahi kuvuka hatua ya robo fainali tangu mwaka 2009, wakati ndoto zao zilipozimwa na Manchester United. Msimu huu majeruhi wengi ya wachezaji muhimu akiwamo Kai Havertz, Bukayo Saka, Gabriel Jesus na Gabriel Martinelli yamekwamisha mipango mingi licha ya kufanya usajili wa wachezaji kama Riccardo Calafiori na Mikel Merino.
Lakini, katika kuelekea dirisha lijalo la usajili wa majira ya kiangazi, kocha Arteta anahitaji kuboresha kikosi chake.
Kipa na mabeki; Inawezekana kuwa na tatizo kwingineko kwenye kikosi, lakini Arsenal inaonekana kuwa imara kwenye safu ya ulinzi. Arteta amekuwa akiwabadili wachezaji wake kwenye safu ya ulinzi kulingana na wapinzani anaokabiliana nao, lakini dhidi ya timu zenye upinzani mkali, amekuwa na kikosi kinachoeleweka.
Kwa maana hiyo, golini ataendelea kubaki kipa David Raya na mabeki wake wa kati ni William Saliba na Gabriel, huku kulia ni Jurrien Timber na kushoto ni Myles Lewis-Skelly. Ben White na Riccardo Calafiori watasubiri kwenye benchi.
-Safu ya kiungo; Jorginho anaondoka kwenda Flamengo, hivyo kwenye eneo hilo Arteta atahitaji kunasa mchezaji mpya baada ya Thomas Partey naye kuwa njia ya panda. Kiungo Martin Zubimendi amekuwa akihusishwa na miamba hiyo ya Emirates, kwamba akanaswa kwenye dirisha lijalo akitokea Real Sociedad, ili kuja kucheza sambamba na Martin Odegaard, Mikel Merino na Declan Rice kwenye eneo hilo la katikati ya uwanja.
-Safu ya ushambuliaji; Arsenal bila ya shaka itaingia sokoni kunasa huduma ya straika mpya kwenye dirisha lijalo na tayari kuna majina ya mastaa wengi wanaohusishwa na timu hiyo ikiwamo Benjamin Sesko, Jonathan David, Alexander Isak na wengine kibao ambao watakuja kuongeza nguvu sambamba na Saka, Havertz, Martinelli, Jesus, Ethan Nwaneri na Leandro Trossard ili kuifanya fowadi ya Arsenal kuwa moto wa kuotea mbali msimu ujao.