Pep Guardiola amtia presha Arteta
Muktasari:
- Guardiola, anayekinoa kikosi cha Manchester City yupo kwenye vita kali ya kuifukuzia Arsenal ya Arteta kwenye kilele cha msimamo wa Ligi Kuu England baada ya timu hizo mbili kutofautiana pointi sita.
MANCHESTER, ENGLAND: PEP Guardiola anatumia mbinu ya nje ya uwanja kumtisha mpinzani wake kwenye mbio za ubingwa Mikel Arteta kwamba hatashinda ubingwa licha ya kutumia pesa nyingi kwenye usajili kuliko yeye.
Guardiola, anayekinoa kikosi cha Manchester City yupo kwenye vita kali ya kuifukuzia Arsenal ya Arteta kwenye kilele cha msimamo wa Ligi Kuu England baada ya timu hizo mbili kutofautiana pointi sita.
Kocha Guardiola alikejeli kwamba anasikitishwa na kukerwa na mabosi wake wa Etihad kutotumia pesa nyingi licha ya miamba hiyo kutumia Pauni 455.8 milioni katika madirisha manne ya mwisho ya usajili. Man City ipo nafasi ya saba kwenye jedwali la matumizi taslimu (net spend) ya klabu za Ligi Kuu England katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Guardiola amesema: “Bahati njema kwa timu sita zilizo mbele yetu kwa matumizi taslimu katika miaka mitano iliyopita. Nataka kuwa wa kwanza. Sielewi kwa nini klabu haitumii pesa zaidi. Nimekasirika kidogo. Kwa nini tusitumie pesa zaidi? Lakini kama tulishinda zamani kwa sababu tulitumia pesa nyingi, basi sasa timu sita lazima zishinde Ligi Kuu, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la FA kwa sababu zimetumia zaidi katika miaka mitano iliyopita.”
Guardiola bado alikuwa anaonekana kukerwa na matokeo ya sare ya 2-2 dhidi ya Tottenham, Jumapili, baada ya Man City kupoteza uongozi wa mabao mawili huku matokeo hayo yakiiacha timu hiyo nyuma kwa pointi sita dhidi ya vinara Arsenal.
Kwenye dirisha la Januari 2026, kikosi hicho cha Man City kimeongeza mastaa wawili wa maana kabisa, ilipomnasa Antoine Semenyo kwa uhamisho wa Pauni 62.5 milioni na Marc Guehi kwa Pauni 20 milioni.
Manchester United inaongoza jedwali la matumizi taslimu katika misimu mitano iliyopita, ikifuatiwa na Arsenal, Chelsea, Tottenham, Newcastle na Liverpool.
Man City imetumia Pauni 455.8 milioni katika madirisha manne ya mwisho ya usajili. Lakini, kwa kipindi cha miaka mitano, matumizi yao taslimu ni chini ya Pauni 300 milioni chini ya nusu ya yale ya wapinzani wao wakuu.