Arteta, Rice watuma salamu baada ya kufuzu fainali
Muktasari:
- Hii itakuwa fainali yao ya kwanza chini ya kocha Mikel Arteta tangu alipowaongoza kutwaa Kombe la FA mwaka 2020 na ni ya pili tu katika kipindi chake akiwa klabuni hapo.
BAADA ya takribani miaka sita ya kusubiri na kushindwa mara nne mfululizo katika hatua ya nusu fainali, ushindi wa Arsenal wa jumla ya mabao 4-2 dhidi ya Chelsea kwenye nusu fainali ya Kombe la Carabao umewarejesha tena kwenye fainali ya mashindano makubwa.
Hii itakuwa fainali yao ya kwanza chini ya kocha Mikel Arteta tangu alipowaongoza kutwaa Kombe la FA mwaka 2020 na ni ya pili tu katika kipindi chake akiwa klabuni hapo.
Mchezo ulikuwa mgumu, wenye presha na wakati mwingine haukuwa na mvuto mkubwa, lakini pale Kai Havertz alipofunga bao katika dakika za majeruhi kuthibitisha tiketi ya kwenda Wembley, shangwe za mashabiki na wachezaji ndani ya Uwanja wa Emirates zilionyesha wazi uzito wa mafanikio hayo.
Katika mechi ambayo kila timu ilipata mashuti mawili tu yaliyolenga lango, Arsenal hawakuonekana kupata tabu kubwa, wakionyesha ubora na nidhamu iliyowafanya kuwa vigumu kuwashinda msimu huu.
Matokeo hayo yanamaanisha Arsenal watashiriki fainali yao ya tisa ya Kombe la EFL, ambapo watakutana na Manchester City au Newcastle United mnamo Jumapili, Machi 22, 2026 katika mchezo wa fainali ya mashindano hayo.
Iwapo watakutana na Manchester City, itakuwa marudio ya fainali ya mwaka 2018 ambapo Arsenal ilipoteza, wakati Arteta akiwa sehemu ya benchi la ufundi la Pep Guardiola.
Zaidi ya kuwa fursa ya kulipiza kisasi kwa kipigo hicho na kutwaa kombe hilo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 33, fainali hiyo pia itakuwa hatua muhimu ya kubadili mtazamo uliopo kuhusu Arsenal.
Akizungumza baada ya mechi, kocha Arteta amesema: “Kulikuwa na hali ya kipekee sana ndani ya uwanja wetu. Inaleta tofauti kubwa. Tumekuwa tukisubiri kwa miaka kadhaa kufikia hatua hii na hakika tutaufurahia mchezo wa fainali.
“Hizi ni kama vitamini bora kabisa kwa miili yetu kwa sababu tunacheza kila baada ya siku tatu. Lakini ukweli ni kwamba tumefanya kazi kwa bidii kufikia nyakati hizi na kuzipitia pamoja ni jambo la kichawi kabisa.
“Unaona furaha, tabasamu, nguvu na kila kitu kinachofanya klabu ifanye kazi vizuri.”
Kiungo wa Arsenal, Declan Rice ameongeza: “Tunastahili. Kwa miaka mitatu au minne iliyopita tumekuwa juu kwenye Ligi Kuu, tukipambana na kukaribia sana, lakini hatujawa bora vya kutosha.
“Ndiyo maana msimu huu tuna kiu ya ziada na moto ndani ya mioyo yetu wa kwenda hatua moja mbele zaidi katika kila mashindano. Bado kuna safari ndefu, lakini kuwa kwenye fainali ya kombe ukiwa na klabu hii ni jambo la ajabu.”
Kwa miaka ya hivi karibuni, enzi ya Arteta, Arsenal imekuwa simulizi ya kukaribia mafanikio bila kuyafikia, iwe kwenye mashindano ya vikombe au kwenye Ligi Kuu.
Sasa, wakiwa umbali wa mchezo mmoja tu kumaliza ukame wa mataji, je, vinara wa Ligi Kuu wanakaribia kuzima kabisa lawama za kuitwa “timu ya karibu kufanikiwa”?
Mlinzi wa zamani wa Arsenal, Matt Upson, ameiambia BBC Radio 5 Live kwamba: “Hili limekuwa jambo la muda mrefu. Kumekuwepo na mchakato wa hatua kwa hatua hadi kufikia hapa. Mikel Arteta amekuwa akiweka misingi, akijenga falsafa, utamaduni na mshikamano wa timu.”