Pauni 57 milioni kumng’oa Bruno Old Trafford, mwenyewe atia neno
Muktasari:
- Bruno mwenye umri wa miaka 31, amekuwa akihusishwa na taarifa za kuondoka Man United kwa muda sasa, huku baadhi ya klabu za Saudi Arabia zikitajwa kumwania.
Imefahamika kuwa, kiungo na nahodha wa Manchester United, Bruno Fernandes, huenda akaondoka kwenye klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu kwa dau la Pauni 57 milioni.
Bruno mwenye umri wa miaka 31, amekuwa akihusishwa na taarifa za kuondoka Man United kwa muda sasa, huku baadhi ya klabu za Saudi Arabia zikitajwa kumwania.
Kwa sasa klabu ya Al-Hilal ya Saudia ndio inatajwa sana katika mpango wa usajili wa kiungo huyo wa Ureno, na inadaiwa kuwa tayari kutoa dau la Pauni 57 milioni, ambalo litafanikisha kumng’oa huko Old Trafford.
Kwenye mkataba wa Bruno na Man United, kipengele cha kuondoka (release clause) kinachoainisha Pauni 57 milioni kama ada yake ya usajili, ambayo itapaswa kulipwa na klabu itakayokuwa tayari kumsajili.
Hata hivyo, Bruno aliwahi kugomea mpango wa kuondoka Old Traffold mwishoni mwa msimu huu, na alipoulizwa kwa nini alichukuwa uamuzi huyo, alisema: “Kama nilivyosema daima, najisikia vizuri hapa Old Trafford. Nataka kufikia ndoto zangu nikiwa hapa."
Kuhusu mpango wa kuondoka mwishoni mwa msimu huu, kiungo huyo amesema: "Nimeona habari nyingi zikizungumzwa kwamba tayari nina makubaliano ya kuondoka msimu ujao. Ikiwa klabu imefanya makubaliano hayo, basi inapaswa kutambulika kwamba hiyo sio kwa upande wangu.
"Hivyo hadi sasa sijazungumza na mtu yeyote. Naweza kukwambia bado kuna watu wanaonipigia simu wakisema wangependa sana kuniona nikiwa nao msimu ujao.
"Lakini kwa upande wangu, hilo halijazungumzwa bado. Maana wakala wangu anajua jinsi ninavyofanya kazi, kwa hiyo kama anataka kuzungumza nami, itakuwa baada ya Kombe la Dunia. Kabla ya hapo sitazungumza na mtu yeyote.
"Swali la kwanza nililomuuliza mke wangu lilikuwa, ‘Tuna ofa hii kutoka Saudi, unaonaje?’ Na jambo la kwanza aliloniambia ni, ‘Je, umefanikisha kila kitu ulichotaka kufanikisha hapa Man United?’ Kwa sababu anajua bado sijafanikisha.
"Ninaposema sijafikia ndoto zangu kwenye klabu, linatokana sana na maneno ya mke wangu. Bila shaka, sina uhakika kama nitafanikiwa, wala yeye hana uhakika. Lakini nisipojaribu, ni wazi sitafanikiwa.”
Fernandes amefunga mabao mawili na kutoa asisti moja katika michezo tisa aliyochezea Man United msimu huu 2025/26.
Manchester United kwa sasa ipo nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi ya EPL, ikiwa na pointi 13 baada ya kucheza mechi nane.