Paul Pogba kucheza ni Inter Miami, Uarabuni

Muktasari:
- Staa huyu ambaye amevunja mkataba wake na Juventus anapewa nafasi kubwa ya kutua Inter Miami ya Marekani ambako ameonekana mara kadhaa akiwa na mmiliki wao David Beckham.
PAUL Pogba ambaye adhabu yake ya kifungo cha kutocheza soka kinamalizika wiki hii, hadi sada bado hajafanya uamuzi wa wapi anaweza kusaini licha ya kupokea ofa kibao kutoka timu mbalimbali.
Staa huyu ambaye amevunja mkataba wake na Juventus anapewa nafasi kubwa ya kutua Inter Miami ya Marekani ambako ameonekana mara kadhaa akiwa na mmiliki wao David Beckham.
Awali kabla ya Inter Miami, fundi huyu ilitajwa kuwa huenda akatimkia Saudi Arabia ambako timu kibao zimeonyesha nia ya kumsajili.
Mara baada ya kumaliza adhabu yake aliyoipata kwa kosa la kutumia dawa zilizokatazwa michezoni, Pogba atakuwa huru kusaini na timu yoyote barani Ulaya bila ya kusubiri dirisha la usajili kwani ni mchezaji huru.
Kobbie Mainoo
CHELSEA imeongeza juhudi katika kuiwania saini ya kiungo wa Manchester United raia wa England, Kobbie Mainoo, 19, inayehitaji kumsajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Chelsea inataka kumsajili Mainoo baada ya staa wao Romeo Lavia, 21, kutompa kocha Enzo Maresca anachohitaji na muda mwingi anaandamwa na majeraha. Mainoo amekuwa akikosa nafasi katika kikosi cha Kocha Ruben Amorim na kuna kila dalili akaondoka.
Eduardo Camavinga
MANCHESTER City inamfuatilia kwa karibu kiungo wa Real Madrid na timu ya taifa ya Ufaransa, Eduardo Camavinga, 22 , ambaye Kocha Pep Guardiola anaamini atakuwa mwarobaini wa tatizo la timu kufikika kirahisi pale Rodri anapokuwa majeruhi. Camavinga ni miongoni mwa wachezaji tegemeo wa kikosi cha kwanza cha Madrid na Man City imepania kutengeneza kikosi chake msimu ujao kwa ajili ya kuwania mataji.
Bruno Guimaraes
ARSENAL imepanga kumsajili kiungo wa Newcastle United na timu ya taifa ya Brazil, Bruno Guimaraes kwa ajili ya kuboresha eneo la kiungo. Bruno anaangaliwa kama mbadala wa Thomas Partey ambaye kuna uwezekano mkubwa akaondoka mwisho wa msimu huu baada ya mkataba wake kumalizika. Mbrazil huyu anaweza kuuzwa kwa zaidi ya Pauni 70 milioni. Manchester City pia inamwania nyota huyo.
Ademola Lookman
ADEMOLA Lookman anatarajiwa kuondoka Atalanta katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi na ameonyesha nia ya kutimkia England ambako Chelsea na Arsenal zimeonyesha mpango wa kutaka kumsajili. Straika huyu wa kimataifa wa Nigeria, anapewa nafasi kubwa ya kuondoka kutokana na mahusiano yake na kocha wa Atalanta, Gian Piero Gasperini kuvurugika.
Samu Aghehowa
Manchester United huenda ikalipa Pauni 84 milioni kwenda FC Porto ili kuipata huduma ya mshambuliaji wa timu hiyo raia wa Hispania, Samu Aghehowa, 20. Samu aliyejiunga na Porto akitokea Atletico Madrid kiasi hicho cha pesa kipo katika mkataba wake kwa timu itakayohitaji kumsajili. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2029 na kuna uwezekano akaondoka.
Fikayo Tomori
BEKI wa kati wa AC Milan Fikayo Tomori ameendelea kubaki sokoni baada ya dili la kutua Juventus na Tottenham kufeli dirisha lililopita la majira ya baridi. Kwa mujibu wa ripoti kutoka Italia, Tomori anaweza kutolewa kwa mkopo au kuuzwa kwa kiasi kisichopungua Euro 20 milioni. West Ham pia inatajwa kumwania.
Theo Hernandez
BEKI wa AC Milan na Ufaransa, Theo Hernandez huenda akauzwa katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi kwa ada ya uhamisho inayofikia Euro 30 milioni baada ya kiwango kibovu alichoonyesha tangu kuanza kwa msimu huu. Mkataba wa sasa wa staa huyu unatarajiwa kumalizika mwakani na hadi sasa hakuna mazungumzo kati yake na Milan juu ya mkataba mpya.