Palmer afanya yake, Chelsea ikitwaa Kombe la Dunia la Klabu
Muktasari:
- Mabao mawili ya Cole Palmer na Joao Pedro yametosha kuipa Chelsea ubingwa huo kwa mara ya pili katika historia yake.
NEW JERSEY, MAREKANI: KOCHA Enzo Maresca na vijana wake wa Chelsea wameandika historia mpya baada ya kuibuka mabingwa wa kwanza wa mfumo mpya mashindano ya fainali za Kombe la Dunia la Klabu kwa kuichapa Paris Saint Germain mabao 3-0 kwenye fainali iliyopigwa katika Uwanja wa MetLife, New Jersey, Marekani.
Cole Palmer ndiye aliyekuwa staa wa mchezo, akiwa msumari wa moto kwa vijana wa Luis Enrique, akifunga mabao mawili na kuasisti bao la tatu lililofungwa na Joao Pedro.
Chelsea ilitumia kasi ya mashambulizi ya kushtukiza. Bao la kwanza la Palmer lilikuja dakika ya 12 baada ya kupokea pasi ya Gusto na kumalizia kwa utulivu mkubwa.
Huku Bao la pili lilifuata dakika ya 20, safari hii likiwa ni matokeo ya juhudi binafsi alipochonga mpira akiwatoka mabeki wa PSG kabla ya kumalizia kwa ustadi mkubwa.
PSG iliopoteza mechi ya makundi dhidi ya Palmeiras ilijaribu kurudi mchezoni kwa kutegemea kasi ya Ousmane Dembélé na akili ya Vitinha, lakini ilikumbana na ukuta imara wa Chelsea ukiongizwa na kipa Robert Sánchez ambaye alifanya kazi ya ziada kuzuia mashambulizi yote.
Dakika ya 35, Palmer alipenya kati ya mabeki wa PSG na kumpasia Pedro ambaye alimzidi maarifa Donnarumma na kuandika bao la tatu, ambalo lilikuwa kama pigo la mwisho kwa matumaini ya Wafaransa hao.
Juhudi za PSG kurejea zilizimwa kabisa na kadi nyekundu aliyonyooshewa kiungo João Neves dakika ya 84 baada ya kumvuta nywele beki Marc Cucurella katika harakati za kumzuia kuanzisha mashambulizi.
Hasira zilionekana wazi kwenye uso wa kocha Luis Enrique, ambaye sasa anapoteza fursa ya kuwa kocha wa kwanza tangu mwaka 2015 (Barcelona) kushinda Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL), Ligi ya ndani, Kombe la ndani na Kombe la Dunia la Klabu kwa msimu mmoja.
Ushindi huu unakuwa wa pili kwa Chelsea kwenye historia ya Kombe la Dunia kwa Klabu, baada ya ule wa mwaka 2021, lakini wa kwanza katika mfumo mpya wa mashindano hayo unaojumuisha klabu nyingi zaidi.
Kwa ushindi huu, Chelsea pia wamejishindia zaidi ya Pauni 90Milioni, pesa ambayo inaweza kuimarisha zaidi kikosi hicho kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu ya England na mashindano ya Ulaya.