FIFA yashusha mpira wa mechi nne
Muktasari:
- Kama uliuona kwenye mchezo wa jana, mpira huo unaoitwa Trionda Final umetambulishwa rasmi na Adidas ukiwa ni toleo maalumu la mpira wa Trionda, uliotumika tangu hatua ya makundi hadi robo fainali za michuano hiyo.
LOS ANGELES, MAREKANI: SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (FIFA), kwa kushirikiana na kampuni ya vifaa vya michezo ya Adidas, limetangaza matumizi ya mpira mpya ulioanza kutumika kuanzia hatua za nusu fainali jana hadi mchezo wa fainali wa Kombe la Dunia 2026.
Kama uliuona kwenye mchezo wa jana, mpira huo unaoitwa Trionda Final umetambulishwa rasmi na Adidas ukiwa ni toleo maalumu la mpira wa Trionda, uliotumika tangu hatua ya makundi hadi robo fainali za michuano hiyo.
Kwa mujibu wa Adidas, Trionda Final umebaki na teknolojia na muundo uleule wa mpira wa awali, lakini umewekewa muonekano mpya unaoakisi umuhimu wa mechi za hatua za mwisho za Kombe la Dunia.
Aidha, muonekano wa mpira huo unaenzi miji minne itakayokuwa mwenyeji wa hatua za mwisho za michuano hiyo ambayo ni Dallas, Atlanta, Miami na New York/New Jersey.
Muundo wake wa rangi za dhahabu, nyeupe na nyeusi umechochewa na Kombe la Dunia la FIFA, huku rangi ya dhahabu ikiakisi hadhi ya kombe hilo na rangi nyeusi ikiupa mpira mwonekano wa kipekee.
Michoro ya pembetatu iliyopo kwenye mpira huo imebeba heshima kwa miji yote 16 iliyokuwa mwenyeji wa michuano hiyo, ikiwa ni kumbukumbu ya safari ya Kombe la Dunia kubwa zaidi kuwahi kufanyika.
Adidas imesema mabadiliko hayo yanalenga kuipa hadhi ya kipekee hatua ya mwisho ya mashindano hayo, ikiwa ni mara ya kwanza kwa FIFA kutumia mpira tofauti kwa mechi za nusu fainali, mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu na fainali ya Kombe la Dunia.
Mpira huo mpya ulitumika katika mechi za nusu fainali kati ya Ufaransa dhidi ya Hispania jana na Argentina dhidi ya England leo, kabla ya kutumika pia katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu na fainali ya Kombe la Dunia 2026.