Palace yakubali kwa Guehi, Barca, Madrid zatajwa
Muktasari:
- Staa huyu anahusishwa na timu mbalimbali Ulaya lakini Liverpool iliyohitaji sana kumsajili dirisha lililopita la majira ya kiangazi inadaiwa kuachana na mpango huo na badala yake sasa Barcelona, Real Madrid na Bayern Munich ndio zinatajwa kutaka kumsajili.
CRYSTAL Palace inajiandaa kumuuza beki wake wa kati wa kimataifa wa England, Marc Guehi dirisha lijalo la majira ya baridi.
Staa huyu anahusishwa na timu mbalimbali Ulaya lakini Liverpool iliyohitaji sana kumsajili dirisha lililopita la majira ya kiangazi inadaiwa kuachana na mpango huo na badala yake sasa Barcelona, Real Madrid na Bayern Munich ndio zinatajwa kutaka kumsajili.
Guehi aliyekulia katika akademi ya Chelsea, amekuwa mhimili wa safu ya ulinzi ya Palace tangu alipojiunga mwaka 2021 akitokea Swansea City kwa dau la takriban Pauni 18 milioni.
Kwa mujibu wa ripoti, beki huyu anatamani sana kutua Real Madrid kwani ni timu ya ndoto yake licha ya kwamba alishafanya hadi makubaliano binafsi na Liverpool katika dirisha lililopita.
Palace iliachana na mpango wa kumuuza staa huyu kwenda kwa Majogoo wa Jiji la Liverpool baada ya kocha wao kutishia kubwaga manyanga ikiwa angeuzwa kwa sababu hakukuwa na muda wa kupata mbadala wake.
Adam Wharton
KIUNGO wa Crystal Palace, Adam Wharton, 21, ni miongoni mwa mastaa ambao wapo katika vipaumbele vya usajili wa Manchester United katika dirisha lijalo la Januari. Taarifa kutoka tovuti ya Teamtalk zinasema Palace huenda wakahitaji zaidi ya Pauni 70 milioni kwa ajili ya kumuuza nyota huyo aliyejiunga nao mwaka jana akitokea Blackburn Rovers kwa Pauni 22 milioni. Manchester United wanamtazama kama mbadala wa muda mrefu wa Casemiro.
Jarrad Branthwaite
EVERTON ilikataa maombi kadhaa kutoka kwa Liverpool na Chelsea zilizokuwa zinahitaji huduma ya beki wao wa kati raia wa England, Jarrad Branthwaite, 23. Everton wanamtazama Branthwaite kama sehemu muhimu ya kikosi chao na hawatokuwa tayari kumuza kwa bei ya chini ya Pauni 80 milioni. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2030, msimu uliopita alicheza mechi 33 za michuano yote.
Antoine Semenyo
TOTTENHAM Hotspur na Liverpool zinamfuatilia kwa karibu winga wa Bournemouth na timu ya taifa ya Ghana, Antoine Semenyo, 25. Kwa mujibu wa tovuti ya Talksport, winga huyo ana kipengele kinachomruhusu kuondoka kwa kiasi maalum cha pesa lakini Bournemouth hawajataja kiasi hicho na wamekuwa wakikanusha kuwepo kwa kipengele. Katika msimu uliopita Semenyo alicheza mechi nane za michuano yote, akafunga mabao sita na kutoa asisti tatu.
Neymar Jr
INTER Milan imepinga vikali uvumi unaoenea kwamba wako karibu kumsajili mshambuliaji wa Brazil Neymar Jr., mwenye umri wa miaka 33, dirisha lijalo. Taarifa kutoka Italia zilidai kwamba Inter walikuwa wanajiandaa kumchukua Neymar bure baada ya mkataba wake na Santos FC kumalizika mwishoni mwa mwaka huu. Hata hivyo, vyanzo vya ndani vya klabu vimeeleza kuwa hakuna mazungumzo yoyote rasmi yaliyofanyika.
Federico Dimarco
KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim, anaripotiwa kuwa shabiki mkubwa wa beki wa kushoto wa Inter Milan na timu ya taifa ya Italia, Federico Dimarco, 27. Kwa mujibu wa Tuttosport, Amorim anaamini Dimarco ana sifa za kipekee zinazoweza kuboresha na kuongeza kitu katika safu yake ya ulinzi. Hata hivyo, Dimarco mwenyewe amefunguka kuwa anajisikia furaha kuendelea kusalia katika viunga vya Inter.
Marc Ter Stegen
KIPA wa Barcelona, Marc-Andre ter Stegen, 33, bado hajafanya uamuzi wa mwisho kuhusu kama ataendelea kukaa klabuni hapo au ataondoka dirisha lijalo. Ter Stegen inadaiwa kutaka kuondoka ili kupata nafasi zaidi ya kucheza ili kuitwa katika mashindano yajayo ya Kombe la Dunia mwaka 2026. Kwa sasa Barca inamtumia zaidi Wojciech Szczesny.
Yan Diomande
RB Leipzig inahitaji Euro 100 milioni ili kumuuza winga wao wa kimataifa wa Ivory Coast, Yan Diomande, mwenye umri wa miaka 18. Kwa mujibu wa tovuti ya Sky Germany, bei hiyo imewekwa ili kuzuia klabu kubwa za Ulaya vinazomfuatilia kijana huyo kutokana na uwezo wake wa hali ya juu. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2030.