Sheria mpya VAR yaanza na Embolo
Muktasari:
- Embolo, ambaye tayari alikuwa ameonyeshwa kadi ya njano kipindi cha kwanza, alitolewa nje dakika ya 72 katika robo fainali dhidi ya Argentina baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kwa tuhuma za kujirusha.
KANSAS CITY, MAREKANI: MSHAMBULIAJI wa Uswisi, Breel Embolo, ameandika historia isiyotamaniwa baada ya kuwa mchezaji wa kwanza kutolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na matumizi ya sheria mpya ya VAR inayoruhusu mwamuzi kubadili utambulisho wa mchezaji aliyeonyeshwa kadi kimakosa katika Kombe la Dunia 2026.
Embolo, ambaye tayari alikuwa ameonyeshwa kadi ya njano kipindi cha kwanza, alitolewa nje dakika ya 72 katika robo fainali dhidi ya Argentina baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kwa tuhuma za kujirusha.
Awali, mwamuzi Joao Pinheiro alimpa kadi ya njano kiungo wa Argentina, Leandro Paredes, akiamini ndiye aliyefanya faulo.
Hata hivyo, baada ya VAR kumtaka kupitia tukio hilo kwenye skrini ya pembeni, mwamuzi alibadili uamuzi wake na kubaini kuwa Embolo alijirusha akitaka kupata faulo, hivyo akamwonyesha kadi ya pili ya njano iliyomtoa nje ya mchezo.
Alitoka uwanjani akilia
Uamuzi huo ulimuumiza mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 29, hasa ikizingatiwa kuwa Uswisi ilikuwa imesawazisha bao dakika tano tu kabla ya tukio hilo dhidi ya mabingwa watetezi.
Embolo alionekana akitoka uwanjani jijini Kansas City akiwa analia, huku akifarijiwa na wachezaji wenzake.
Kocha Yakin alalamikia sheria
Kocha wa Uswisi, Murat Yakin, hakuficha hasira yake baada ya mchezo, akidai sheria hiyo imeharibu mpira wa miguu.
"Hakukuwa na sababu yoyote ya kutoa kadi ya njano. Lilikuwa tukio la kawaida kabisa na mwamuzi alipaswa kuendelea na mchezo," amesemaYakin.
Ameongeza:"Tumeadhibiwa na sheria ambayo siikubali kabisa. Sielewi kwa nini VAR iliingilia tukio kama lile. Ni sheria ambayo haina uhusiano na mpira wa miguu. Imeharibu mchezo wetu. Tunalazimika kuukubali uamuzi huo, lakini inauma kupoteza kwa namna hii."
Wachambuzi wamlaumu Embolo
Licha ya malalamiko ya kocha wake, wachambuzi wengi hawakuwa na huruma kwa Embolo.
Mshambuliaji wa zamani wa Major League Soccer (MLS), Bradley Wright-Phillips, alisema:"Nawaonea huruma wachezaji wenzake, lakini si Embolo. Ameigharimu timu yake nafasi ya kufika nusu fainali."
Naye mchezaji wa zamani wa Jamaica, Jobi McAnuff, alisema:"Breel Embolo ameiangusha timu yake. Mwendo wa taratibu kwenye marudio ya video ulifanya ionekane wazi kwamba alijirusha. Labda alidhani angeguswa mapema, lakini haikutokea. Ni kujirusha, ingawa bado unamhurumia."
Argentina yatumia nafasi hiyo
Ikiwa na mchezaji mmoja zaidi uwanjani, Argentina ilitumia vyema faida hiyo na kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 baada ya dakika za nyongeza, na sasa itavaana na England katika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia.
Licha ya kuondolewa, Yakin aliwasifu wachezaji wake kwa kupambana hadi mwisho.
"Timu hii ina moyo mkubwa. Hata tulipobaki pungufu kwa mchezaji mmoja, tuliendelea kupigana hadi mwisho. Ninajivunia kila mmoja wao," amesemakocha huyo.