Onana, Ederson kuziingiza vitani Man United, Man City

Muktasari:
- Hata hivyo, ili kupata mbadala wa Onana, Man United huenda ikatumia kiasi kikubwa cha pesa ili kufanikisha hilo kwani itatakiwa kushinda vita dhidi ya timu nyingine kubwa ambazo zitakuwa sokoni kutafuta makipa katika dirisha lijalo ikiwemo Manchester City.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER UNITED wako tayari kumuuza kipa wao namba moja Andre Onana kwenda Saudi Arabia katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ikiwa ni katika mpango wa kocha wao Ruben Amorim kusuka upya kikosi hicho.
Hata hivyo, ili kupata mbadala wa Onana, Man United huenda ikatumia kiasi kikubwa cha pesa ili kufanikisha hilo kwani itatakiwa kushinda vita dhidi ya timu nyingine kubwa ambazo zitakuwa sokoni kutafuta makipa katika dirisha lijalo ikiwemo Manchester City.
Timu hizi mbili zote zinatarajiwa kuuza makipa wao mwisho wa msimu ambapo Ederson kwa upande wa Man City naye anatarajiwa kwenda Saudi Arabia.
Guardiola na Amorim wameshaanza kutafuta makipa wanaoweza kuchukua nafasi hizo na kuna baadhi ya majina yametokea katika ripoti zote za makocha hao.
Kipa wa kwanza anatajwa kuwa ni Senne Lammens kutoka Royal Antwerp ambaye pia anawindwa na timu nyingine za England ikiwemo Newcastle na West Ham.
Wa pili ni kipa wa Lille, Lucas Chevalier, mwenye umri wa miaka 23, ambaye maskauti wa Man United wamekuwa wakimfuatilia kwa miezi kadhaa iliyopita.
Lammens, mwenye umri wa miaka 22, anakadiriwa kuwa huenda akauzwa kwa kiasi kisichopungua Pauni 30 milioni.
Hivi karibuni alichaguliwa katika kikosi cha Ubelgiji licha ya kutokuwa na uzoefu wa kutosha lakini amekuwa na ubora mkubwa linapokuja suala kucheza mpira kwa miguu staili ambayo Guardiola anapenda kuiona kwa makipa.
Kwa upande wa ambaye ana mkataba hadi mwaka 2027, vyanzo kutoka Ufaransa vinadai Lille ipo tayari kumuuza kwa Pauni 40 milioni. Msimu huu Onana amekuwa akifanya makosa mengi.