Oklahoma City Thunder watabeba ubingwa NBA?

Muktasari:
- Hii imeifanya kuwa timu ya kwanza kufanya hivyo msimu huu na kuwa miongoni mwa timu zinazopigiwa chapuo kutwaa ubingwa wa NBA msimu huu.
OKLAHOMA, MAREKANI: Oklahoma City Thunder ndiyo inayotawala Ukanda wa Magharibi msimu huu wa 2024-25 na hadi sasa na imefikia ushindi wa mechi 60.
Hii imeifanya kuwa timu ya kwanza kufanya hivyo msimu huu na kuwa miongoni mwa timu zinazopigiwa chapuo kutwaa ubingwa wa NBA msimu huu.
Hata hivyo, mafanikio haya yataendelea hadi kwenye hatua za mtoano (playoffs)? Kwa uelekeo wa sasa, Thunder imeonyesha si timu ya kubahatisha, bali ni kikosi kilichojengwa kwa msingi madhubuti.
Wanacheza kwa umoja, wana vipaji vya hali ya juu na wana ulinzi mkali unaowafanya kuwa moja ya timu bora zaidi msimu huu. Lakini je, hayo yote yanatosha kuwapa taji lao la kwanza la NBA?
UBORA OKLAHOMA
Mchambuzi Steve Aschburner anasema msimu huu umekuwa wa kipekee kwa Thunder na hakuna sababu ya kudhani hawawezi kuendeleza mafanikio yao hadi playoffs. Kwa mara ya kwanza katika historia yao, wanashikilia rekodi ya kushinda mechi 60 mapema zaidi kuliko timu yoyote nyingine msimu huu.
Sababu kubwa ya mafanikio yao ni uundwaji wa kikosi chenye wachezaji wengi wenye uwezo wa kubadilika kulingana na mbinu mbalimbali za wapinzani wao. Usajili wa Isaiah Hartenstein ulikuwa wa thamani kubwa, kwani ameongeza uimara kwenye safu yao ya ulinzi, hasa akishirikiana na Chet Holmgren katika nafasi ya viungo wa kati.
Mchezaji wao tegemeo, Shai Gilgeous-Alexander, amekuwa na msimu wa kuvutia na anaonekana kuwa mmoja wa wanaowania tuzo ya Kia MVP. Akiwa na umri wa miaka 26, Shai ameonyesha uwezo mkubwa wa kufunga pointi muhimu, jambo linalomfanya kulinganishwa na Dwyane Wade wa fainali za mwaka 2006. Ikiwa ataendelea na kiwango hiki katika playoffs atakuwa mchezaji muhimu na anayeibeba Thunder.
KIZAZI KIPYA
Kwa mujibu wa Brian Martin, Thunder huenda ikawa ni mwendelezo wa enzi mpya kama Golden State Warriors ya miaka ya hivi karibuni au San Antonio Spurs ya miaka ya 2000.
Ingawa ni moja ya timu zenye umri mdogo zaidi (wastani wa miaka 24.1), imekuwa bora zaidi Ukanda wa Magharibi tangu Novemba 25, 2024. Mbali na kuwa na mchezaji anayeongoza katika mbio za MVP (Shai Gilgeous-Alexander), Thunder inakaribia kuvunja rekodi ya muda wote ya NBA kwa tofauti ya wastani wa pointi kwa kila mchezo (+12.9).
Kitu kingine cha kushangaza ni imefanikiwa haya yote ikiwa ni moja ya timu inayolipa mishahara ya chini zaidi katika NBA. Pia, inamiliki chaguzi nyingi za drafti, jambo linalowapa uwezo wa kuimarisha kikosi chao siku za baadaye. Hii inamaanisha Thunder imejengwa kushinda sasa na kuwa timu ya kutisha kwa miaka mingi ijayo.
UZOEFU SASA
Mchambuzi Shaun Powell anaamini ushindi wa mechi 60 ni kipimo kizuri cha ubora wa timu yoyote na Thunder inastahili kuchukuliwa kama washindani halisi wa ubingwa wa NBA.
Licha ya mafanikio yao makubwa, kuna wasiwasi kuhusu kama itaweza kuhimili presha ya hatua za mwisho za playoffs. Uzoefu katika mechi za mchujo ni jambo muhimu sana, hasa unapokabiliana na timu ambazo zimezoea mazingira hayo. Je, kikosi hiki kipya kinaweza kuvumilia presha ya kushindania taji dhidi ya timu kama Denver Nuggets, Boston Celtics, au Milwaukee Bucks?
John Schuhmann anasema Thunder inajitengenezea historia, kwa kuwa na wastani bora wa tofauti ya pointi kwa kila mchezo katika historia ya NBA. Ingawa mashaka kuhusu utendaji wao katika playoffs yapo, wanayo nafasi ya kuwa wao ni timu ya ubingwa kweli.