Nyota wa Barcelona kutimkia PSG
Muktasari:
- Torres mwenye umri wa miaka 26 kwa sasa yupo kambini na timu ya taifa ya Hispania inayoshiriki Kombe la Dunia, ambapo imefuzu hatua ya nusu fainali na inatarajiwa kuvaana na Ufaransa katika mechi yenye mvuto mkubwa.
PARIS, UFARANSA: MSHAMBULIAJI wa Barcelona, Ferran Torres anatarajiwa kujiunga na mabingwa wa Ulaya Paris Saint-Germain (PSG) mara baada ya kumalizika kwa Kombe la Dunia 2026.
Torres mwenye umri wa miaka 26 kwa sasa yupo kambini na timu ya taifa ya Hispania inayoshiriki Kombe la Dunia, ambapo imefuzu hatua ya nusu fainali na inatarajiwa kuvaana na Ufaransa katika mechi yenye mvuto mkubwa.
Inaelezwa kuwa mshambuliaji huyo hatarudi Catalunya baada ya mashindano hayo yanayoendelea Marekani, Mexico na Canada kumalizika.
Mtaalamu wa masuala ya usajili, Gianluca Di Marzio, ameripoti kuwa tayari Torres amefikia makubaliano ya awali na PSG, mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, kwa ajili ya kuhamia jijini Paris.
Mkataba wa Torres na Barcelona unamalizika mwaka 2027, lakini uwezekano wa kuongeza mkataba huo unaonekana kuwa mdogo kwa sasa.
Sababu kubwa ni kwamba Barcelona ipo hatua za mwisho kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa Borussia Dortmund, Karim Adeyemi ambaye ameonekana kuwa mbadala wa muda mrefu katika safu ya ushambuliaji ya klabu hiyo.
Kwa upande wa PSG, wanahitaji kuziba pengo lililoachwa na Goncalo Ramos, ambaye ameripotiwa kuhamia AC Milan, hivyo Torres ameonekana kuwa chaguo sahihi la kuimarisha safu yao ya ushambuliaji.
Torres alijiunga na Barcelona mwaka 2022 akitokea Manchester City, ambako alicheza kwa misimu miwili.
Tangu avae jezi ya miamba hiyo ya Catalunya, amefunga mabao 65 na kutoa pasi 23 za mabao katika mechi 207 alizoichezea klabu hiyo.
Katika kipindi hicho pia amesaidia Barcelona kutwaa mataji matatu ya La Liga pamoja na Kombe la Mfalme (Copa del Rey).
Endapo dili hilo litakamilika, Torres ataungana tena na kocha wa PSG, Luis Enrique, ambaye aliwahi kumfundisha katika timu ya taifa ya Hispania kwa takribani miaka miwili tangu mshambuliaji huyo alipoanza kuchezea timu ya wakubwa mwaka 2020.
Mbali na uhusiano wa kisoka, Torres pia aliwahi kuwa karibu na familia ya Luis Enrique baada ya kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na binti wa kocha huyo, Sira Martinez, kabla ya wawili hao kuachana mwaka 2023.
Kwa sasa, Torres anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Hispania kitakachocheza dhidi ya Ufaransa katika nusu fainali itakayopigwa Jumanne kwenye Uwanja wa AT&T mjini Dallas, Texas, ambapo huenda akaanzia benchi kama ilivyokuwa katika mechi tano zilizopita za Hispania kwenye mashindano hayo.