Hispania yazinduka, ikiishushia kipigo kizito Saudia
Muktasari:
- Dakika 45 za kwanza, zilitosha kuihakikishia ushindi huo Hispania, zikimalizika kwa kufanikiwa kupata mabao matatu.
Hispania imerudisha heshima yake kibabe, baada ya kuichapa Saudi Arabia mabao 4-0 kwenye mchezo wake wa pili hatua ya makundi kwenye Fainali za Kombe la Dunia 2026.
Dakika 45 za kwanza, zilitosha kuihakikishia ushindi huo Hispania, zikimalizika kwa kufanikiwa kupata mabao matatu.
Kiungo Lamine Yamal ambaye kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Cape Verde alitokea benchi, leo ameanza na dakika ya 10 akaipa Hispania bao, akimalizia krosi safi ya Mikel Oyarzabal.
Oyarzabal akapiga mabao mawili dakika ya 21 akitumia asisti ya Aymeric Laporte, lingine akiweka wavuni dakika ya 24 akimalizia asisti ya Dani Olmo, akinufaika na makosa ya beki Saud Abdulhamid, aliyechelewa kuokoa.
Kipindi cha pili Hispania ikaendelea kutawala mchezo ikipata bao la nne dakika ya 49 lililotokana na kujifunga kwa beki wa Saudia, Hassan Tambakti.
Saudia ikapiga shuti pekee lililolenga lango dakika ya 81 kupitia Abdullah Al Hamdan lakini kipa wa Hispania, Unai Simon akadaka vizuri.
Dakika ya 90+2, Hispania ilikaribia kupata bao la tano kupitia mshambuliaji Ferran Torres lakini likafutwa baada ya video ya kumsaidia mwamuzi (VAR) kumnasa na mtego wa kuotea
Hispania ambayo mchezo wa kwanza ililazimishwa sare isiyo na mabao dhidi ya Cape Verde, leo imemaliza dakika 90 kwa ushindi wa mabao 4-0, ikirudisha tabasamu la mashabiki wake.
Ushindi huo unaipeleka Hispania mpaka juu ya msimamo wa Kundi H ikifikisha pointi nne, ikisubiri mchezo wa pili mwingine wa kundi hilo, utakaowakutanisha Uruguay dhidi ya Cape Verde zenye pointi moja kila moja.