Noma sana! Saudia ilivyobadili msimamo wa mishahara mikubwa duniani

RIYADH, SAUDI ARABIA. DIRISHA la usajili la majira ya kiangazi huko Ulaya kwa mwaka huu limeshuhudiwa mastaa kadhaa wenye majina makubwa wakizipa kisogo ligi za huko na kutimka, wengi wakielekea Saudi Arabia na wachache Marekani.
Kwenye jambo hilo, Ligi Kuu tano bora zote za Ulaya kwa maana ya Ligi Kuu England, La Liga, Bundeslia, Serie A na Ligue 1 (ambayo hata hivyo msimu huu imeondolewa kwenye ligi tano bora), zote zimetingishwa.
Kutokana na hilo, msimamo wa wanasoka wanaolipwa pesa ndefu kwa sasa umebadilika, ambapo Saudi Arabia inafunika huku kukiwa na timu moja tu ya Ulaya, Paris Saint-Germain iliyofanikiwa kuwa na mchezaji kwenye orodha ya wakali 10 wanaolipwa mishahara mikubwa kwa mwaka. Lakini, mastaa wengine wote waliobaki ni wale wanaokipiga Saudi Arabia na mkali mmoja kutoka Marekani.
10. Kalidou Koulibaly - Al-Hilal, Euro 30 milioni
Chelsea imekuwa na zaidi ya furaha baada ya kufanikiwa kuachana na beki wao wa kati, Msenegali, Kalidou Koulibaly, ambaye wakati anakipiga Napoli alikuwa moto kwelikweli kabla ya kutua kwenye Ligi Kuu Rngland. Mwaka mmoja tu kati ya miaka minne aliyosaini kuichezea Chelsea, miamba hiyo ya Stamford Bridge imeamua kumpiga bei kwenda Al-Hilal kwa ada ya Pauni 15 milioni. Dili hilo ni biashara tamu kwa Koulibaly, ambaye sasa kwa mwaka analipwa Euro 30 milioni.
9. Riyad Mahrez - Al-Ahly, Euro 35 milioni
Winga wa kimataifa wa Algeria, Riyad Mahrez baada ya kubeba mataji matatu makubwa ndani ya msimu mmoja alipokuwa na kikosi cha Manchester City, mkali huyo ameamua kutimkia zake Saudi Arabia kwenda kupiga pesa ndefu. Mahrez, wakati anakipiga Man City alikuwa akilipwa mshahara wa Pauni 7.8 milioni kwa mwaka, lakini kwa dili lake la kwenda huko Al-Ahly linamshuhudia akipiga pesa ya maana, Euro 35 milioni kwa mwaka na kuwa kwenye orodha ya mastaa matajiri.
8. Sadio Mane - Al-Nassr, Euro 40 milioni
Baada ya msimu mmoja tu kwenye kikosi cha Bayern Munich akitokea Liverpool, supastaa wa kimataifa wa Senegal, Sadio Mane, naye ameamua kutua zake kwenye soka la Saudi Arabia kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi. Mane, huko Saudia amekwenda kujiunga na Cristiano Ronaldo kwenye timu moja huku akipiga pesa ndefu, kutokana na kulipwa Euro 40 milioni kwa mwaka, tofauti na alivyokuwa Bayern Munich, ambako alikuwa akilipwa Euro 22 milioni kwa mwaka.
7. Jordan Henderson - Al-Ettifaq, Euro 40 milioni
Kiungo Mwingereza, Jordan Henderson uhamisho wake wa kwenda Saudi Arabia ulishtua wengi, lakini unaambiwa hivi hakuna mkate mgumu mbele ya chai, pesa zilimfanya staa huyo wa Anfield kung’oka kwenye timu hiyo. Kwenye kikosi cha Liverpool, Henderson mshahara wake kwa mwaka alikuwa akilipwa Pauni 9 milioni, tarakimu moja tu, lakini huko kwenye kikosi cha Al-Ettifaq, kinachonolewa na mkali wa zamani wa Liverpool, Steven Gerrard, analipwa kwa mwaka Euro 40 milioni.
6. Lionel Messi - Inter Miami, Euro 45 milioni
Ligi Kuu Marekani wanadhani wanamlipa pesa nyingi sana mchezaji mahiri wa muda wote, Lionel Messi ili kwenda kucheza kwenye timu yao, lakini ukweli wanachofanya Saudi Arabia ni kufuru zaidi. Supastaa, Messi alijiunga na Inter Miami inayomiliwa na mwanasoka wa zamani, David Beckham aliyojiunga nayo kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi na huko mshahara wake kwa mwaka ni Euro 45 milioni. Alipokuwa PSG kwa mwaka alilipwa Pauni 35.6 milioni.
5. Kylian Mbappe - PSG, Euro 70 milioni
Mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa, Kylian Mbappe ameamua kubaki zake Paris Saint-Germain na kugomea dili tamu kabisa la kutoka kwenye klabu ya Saudi Arabia. Mpango wa staa huyo ni kwenda kujiunga na Real Madrid mwakani wakati mkataba wake utakapofika tamati huko Parc des Princes. Hata hivyo, Mbappe hayupo vibaya mfukoni, amekataa dili tamu la Saudia, lakini PSG wanamlipa vizuri, Euro 70 milioni kwa mwaka na kumfanya awe mmoja wa wanasoka mabosi.
4. N’Golo Kante - Al-Ittihad, Euro 100 milioni
Kiungo Mfaransa, N’Golo Kante kwa miaka mitatu ya karibuni muda mwingi wa soka lake alikuwa nje ya uwanja kutokana na kusumbuliwa sana na majeraha ya mara kwa mara. Lakini, kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi aliachana na Chelsea baada ya mkataba wake kufika mwisho, mahali ambako alikuwa akilipwa Pauni 15 milioni kwa mwaka kabla ya kodi. Lakini, sasa amekwenda kujiunga na Al-Ittihad ya Saudia na kulipwa zaidi ya Euro 100 kwa mwaka.
3. Neymar - Al-Hilal, Euro 100 milioni
Paris Saint-Germain ilishusha pumzi walau baada ya kupata mkwanja wa maana kwa kumpiga bei supastaa wa Kibrazili, Neymar, ambaye alikuwa akilipwa pesa nyingi sana kwenye kikosi chao kwa mwaka. Kwenye mauzo ya Neymar kwenda klabu ya Al-Hilal, PSG imevuna karibu Pauni 80 milioni kwenye ada yake ya uhamisho, lakini dili hilo likimfanya mkali huyo kwenda kupiga pesa ndefu huko Saudia, ambako kinachoelezwa kwa mwaka atakuwa anapokea zaidi ya Euro 100 milioni.
2. Karim Benzema - Al-Ittihad, Euro 200 milioni
Straika Karim Benzema alitua kwenye soka la Saudi Arabia kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi na kwenda kujiunga na timu ya Al-Ittihad. Huo ni usajili mkubwa na ulioacha pengo huko kwenye ligi ya Hispania (La Liga), kwa sababu ndiye mshindi wa tuzo ya Ballon d’Or kwa sasa. Benzema alimaliza mkataba wake Real Madrid, ambako anaripotiwa alikuwa akilipwa Pauni 14 milioni kwa mwaka na sasa ametua Saudia na kulipwa Euro 200 milioni kwa mwaka.
1. Cristiano Ronaldo - Al-Nassr, Euro 200 milioni
Staa wa kwanza mwenye jina kubwa kabisa kuhamia kwenye soka la Saudi Arabia. Supastaa, Cristiano Ronaldo alikuwa akilipwa Pauni 25 milioni kwa mwaka huko Manchester United, lakini baada ya kutibuana na kocha Erik ten Hag na kufanya mahojiano yaliyowachefua mabosi wa klabu hiyo waliamua kumwondoa kikosini na kupata dili la kwenda Al Nassr ya Saudi Arabia, ambako analipwa Euro 200 milioni kwa mwaka.