Ni mapenzi tu, Bruno haoni

Muktasari:
- Ni shairi unaloweza kuliimba baada ya kuona pesa ambazo staa wa Manchester United Bruno Fernandes amezikataa kutoka kwa Waarabu wa Saudi Arabia, Al-Hilal.
ALIWAHI kuandika mwana mashairi gwiji nchini marehemu Shaaban Robert kwamba "Halina kificho penzi liingiapo, mwenye mapenzi haoni ingawa anayo macho".
Ni shairi unaloweza kuliimba baada ya kuona pesa ambazo staa wa Manchester United Bruno Fernandes amezikataa kutoka kwa Waarabu wa Saudi Arabia, Al-Hilal.
Ngoja kwanza! Bruno amekataa ofa ya Pauni 200 milioni kama mshahara ambao angeupata kwa miaka mitatu. Huo hauna kodi wala makato ya aina yoyote, kwa hesabu alikuwa anaenda kukunja Pauni 700,000 kila wiki.
Ndio amekataa. Nimesikiliza mahojiano yake akielezea kwanini amekataa, alijibu tu kirahisi kwamba bado anataka kuendelea kucheza soka la kiushindani. Wikipedia inanionyesha kwamba staa huyu ana miaka 30 na amekuwepo katika soka la kiushindani kwa zaidi ya miaka 10 sasa.
Inafikirisha kidogo. Kukataa huko, huenda kukawa kunatuumiza mioyo zaidi mimi na wewe kuliko yeye aliyekataa ofa hiyo ya mamilioni kutoka kwa Waarabu waliotaka kupata huduma yake, lakini hii isikushangaze sana.
Niliwahi kumsikia Eden Hazard mara baada ya kustaafu soka, alipofanya mahojiano na wakongwe kama Rio Ferdinand, ambapo aliweka wazi kwamba wakati anaondoka Real Madrid na kuamua kustaafu, waarabu walimuwekea mezani ofa ya mshahara wa Pauni 1 milioni kwa wiki, akakataa.
Inawezekana ungemuelewa zaidi Hazard kwa kuwa alitoa sababu kwamba pesa haikuwa shida sana kwake kwani alishapata za kutosha akiwa na Madrid alikokuwa akikunja Pauni 400,000 kwa wiki.
Inawezekana ni mahaba ndio yaliyosababisha Bruno akatae ofa hiyo na kuamua kusalia Man United, stori yake pengine inafanana na ile ya Inaki Williams na Athletic Bilbao yake. Alishafunga mjadala wa kwamba hataondoka katika timu hiyo hata ikiwaje, kwanini? Ni timu iliyowatoa mavumbini na kuwapa maisha ambayo hawakuyatarajia yeye na familia yake wakiwa kama wakimbizi ndani ya Hispania.
Wakati fulani, Sir Alex Ferguson aliwahi kupiga hodi, AC Milan akaulizia uwezekano wa kumpata Paulo Maldini, baba mzazi wa mchezaji huyu alitoa kauli moja tu, 'kama mimi niliwahi kucheza timu tofauti na Milan basi mtoto wangu naye atacheza, lakini kama sikuwahi, mtoto wangu naye hatowahi', hadithi ya Maldini ikaishia Milan hadi anastaafu soka.
Licha ya ukweli kwamba Man United ilikuwa tayari kutoa pesa nyingi zaidi ya zile alizokuwa anazipata Maldini akiwa na Milan, ilishindikana, shida haikuwa pesa, shida ilikuwa ni mahaba.
Bruno anaingia katika mkumbo huu. Kuna muda wachezaji hawachezi tu kwa sababu ya pesa lakini kwa sababu ya mapenzi ya timu wanazochezea.
Wakati Lionel Messi anaondoka Barcelona Agosti 2021 katika mahojiano yake ya kuaga alikuwa akiangusha machozi, aliweka wazi kwamba alikuwa tayari hata kupokea mshahara wa chini ili tu abaki Barca lakini ilishindikana, mahaba yalizidi.
Toni Kroos wakati anastaafu moja kati ya mambo aliyoyasema ilikuwa ni hakuwa anataka kuichezea timu nyingine yoyote baada ya kuondoka Real Madrid, ndio maana timu hiyo ilipoamua kutompa mkataba mpya akaamua kuachana na soka. Ajabu hii! Kwa kiwango chake angeweza kupata timu kubwa barani Ulaya au hata kule kwa Waarabu, lakini hilo halikuwa katika moyo wake. Moyo wake uliandamwa na rangi nyeupe. Moyo wake ulipigwa muhuri wa Madrid.
Inawezekana kuna wanaompongeza na kumkashifu Bruno, lakini kwake yeye huo ni uchaguzi bora katika maisha, kilichomsukuma ni mapenzi kuliko kitu chochote.
Pia ameongeza kwamba ili aondoke Man United ni pale klabu hiyo itakapomwambia kwamba imetosha na hana nafasi tena.