Ngoma ngumu shtaka moja la Diddy

Muktasari:
- Kesi dhidi ya Diddy, mwanamuziki mkongwe wa hip hop ilifunguliwa zaidi ya miaka mitatu iliyopita na miezi michache iliyopita alikamatwa na kuwekwa mahabusu wakati mahakama ikijiandaa kuanza usikilizaji.
NEW YORK, MAREKANI: MAHAKAMA ya New York, Marekani imeanza kusikiliza kesi inayomkabili mwanamuziki nyota, Sean 'Diddy' Combs, huku jopo la baraza la mahakama likifikia uamuzi kuhusu mashtaka manne kati ya matano yanayomkabili.
Kesi dhidi ya Diddy, mwanamuziki mkongwe wa hip hop ilifunguliwa zaidi ya miaka mitatu iliyopita na miezi michache iliyopita alikamatwa na kuwekwa mahabusu wakati mahakama ikijiandaa kuanza usikilizaji.
Usiku wa kuamkia leo, jopo hilo limetangaza kufikia uamuzi katika mashtaka manne, lakini limejizuia kuutangaza hadharani mpaka shtaka kubwa na la mwisho la njama za uhalifu wa kupanga litakapoamuariwa.
Diddy anashtakiwa kwa tuhuma zinazohusiana na usafirishaji wanawake kwa ajili ya ngono na utumikishaji katika vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanawake.
Jopo hilo limeamua kuendelea kujadili shtaka kubwa ambalo pia linadaiwa kwamba limeleta mgawanyiko miongoni mwao.
Jopo linahusisha waendesha mashtaka, mawakili wa Diddy na Jaji Arun Subramanian.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mahakamani jopo hilo limekubaliana kuwa baada ya siku mbili za majadiliano bado ni mapema kukata tamaa kufikia uamuzi kamili kwa ajili ya mashtaka yote.
Na badala ya kutoa sehemu ya uamuzi, Jaji Subramanian ameamuru jopo hilo kuendelea na majadiliano kuhusu shtaka lililobaki. Majadiliano hayo yanatarajiwa kuendelea leo.
Awali, jana usiku jopo liliwasilisha mahakamani ujumbe likisema halijafikia uamuzi wa pamoja kuhusu shtaka la njama za uhalifu wa kupanga kwa sababu baadhi ya wajumbe walikuwa na misimamo mikali na isiyobadilika.
Shtaka la njama za uhalifu wa kupanga ndilo gumu zaidi kwa sababu linalitaka jopo hilo kuamua si tu kama Diddy alikuwa anaendesha genge la kihalifu, bali pia alihusika kutekeleza makosa kama utekaji nyara.
Hata hivyo, ndani ya saa 13 tu za majadiliano, jopo juzi lilifanikiwa kufikia uamuzi kuhusu mashtaka mawili ya usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya ngono na mawili ya kuwasafirisha wanawake kwa nia ya kufanya ukahaba — mashtaka yanayohusisha madai ya kupanga kusafirisha wanawake na watoa huduma za ngono kuvuka mipaka ya majimbo ya Marekani.
Iwapo Diddy atapatikana na hatia, shtaka la usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya ngono lina adhabu ya chini ya kifungo cha miaka 15 jela na juu ni kifungo cha maisha.
Shtaka la kusafirisha wanawake kwa ajili ya ukahaba ni kifungo cha miaka 10 jela, ilhali shtaka lililobaki — na ndilo zito zaidi linaweza kumhukumu kifungo cha maisha gerezani endapo atapatikana na hatia.
Katika kikao cha kusikiliza taarifa ya jopo, Diddy alionekana mwenye huzuni, huku mawakili wake wakizungumza naye na wakati mmoja alichukua karatasi kutoka kwa wakili wake Marc Agnifilo na kuisoma kwa makini.
Baada ya jopo kuingia kupokea taarifa na kisha kutoka, Diddy alikaa kwenye kiti chake kwa dakika chache akiwa kimya na aliposimama kuondoka aliwaangalia ndugu na marafiki waliokuwepo akawapungia busu la mbali na kugusa kifuanie — ishara ambayo aamekuwa akiifanya kila asubuhi na jioni ya siku ya kesi hiyo.
Kabla ya kutoka mahakamani alimsogelea mama yake wakazungumza maneno machache akimalizia kumwambia, “nakupenda” na “nitakuwa sawa”. Kisha askari wa mahakama wakamsindikiza kutoka mahakamani.
Diddy anayefahamika pia kama Sean Combs alishakana ashtaka yote. Mawakili wake wanadai waendesha mashtaka wanajaribu kugeuza maisha yake ya mapenzi ya mabadiliko (swinger lifestyle) kuwa kosa la jinai, na kwamba hata kama kuna chochote kingehesabika kama unyanyasaji wa kifamilia, siyo makosa ya jinai ya kiwango cha kitaifa.