Neymar na dada’ke imetokea tena

Muktasari:
- Siku ya kuzaliwa mrembo Rafaella ni Machi 11 na Neymar alishindwa kuitumikia timu yake ya Santos kwa mara ya kwanza tangu alipojiunga nayo hivi karibuni, lakini lilikuwa tukio la 10 supastaa huyo wa zamani wa Barcelona, Paris Saint-Germain na Al Hilal akikosa mechi kwenye 'birthday' za dada yake.
SANTOS, BRAZIL: GUNDU la siku ya kuzaliwa dada yake Neymar limemkumba tena supastaa huyo wa Kibrazili ambapo kwa mara ya 10 fowadi huyo anakosa mechi na kushindwa kutumikia timu yake kwenye siku ya sherehe ya kuzaliwa kwa dada yake, mrembo Rafaella Santos.
Siku ya kuzaliwa mrembo Rafaella ni Machi 11 na Neymar alishindwa kuitumikia timu yake ya Santos kwa mara ya kwanza tangu alipojiunga nayo hivi karibuni, lakini lilikuwa tukio la 10 supastaa huyo wa zamani wa Barcelona, Paris Saint-Germain na Al Hilal akikosa mechi kwenye 'birthday' za dada yake.
Na jambo hilo limekuwa kama kichekesho kwenye soka kwa Neymar kupata majeraha au kutumikia adhabu kila kipindi kinafikia sherehe hiyo ya kuzaliwa kwa dada yake. Na bado haifahamiki kama staa huyo wa Kibrazili anafanya makusudi kwa ajili ya kuwa na dada yake kusherehekea naye pamoja.
santos ilikuwa na mechi ya ugenini kumenyana na Corinthians, Jumapili, lakini hiyo ilikuwa mara ya 10 kati ya 11 zilizopita kwa mchezaji huyo kukosa mechi kwenye siku za kukaribia siku ya kuzaliwa ya mrembo Rafaella, ambaye ni dada yake. Hivyo, Neymar alikosa mechi hiyo ya nusu fainali ya Campeonato Paulista ambapo kikosi chake kilichapwa na Corinthians.
Neymar, 33, alisema alikosa mechi hiyo kwa sababu hakuwa anajisikia vizuri. Hii imekuwa kawaida kwa Neymar kukosekana kwenye mechi za kukaribia Machi 11 tangu mwaka 2014.
Amekuwa akikosa mechi kwa kuwa na adhabu ya kadi, lakini mara nyingi amekuwa akikosa kwa kuwa majeruhi kwa maumivu ya misuli ambayo huwa inakosa maelezo ya kutosha.
Hata hivyo, kocha wa Santos, Pedro Caixinha alimtetea Neymar kukosa mechi hiyo na kusema: "Kazi yetu ni kufanya kila kitu kuhakikisha tunamlinda Neymar asipate maumivu. Kutojisikia vizuri sio majeraha. Hakuwa kwenye wakati mzuri wa kuonyesha ubora wake. Hivyo, hatutaki kuanza kuzungumza vitu ambavyo havipo."