Newcastle yapewa Man City Carabao, Chelsea ikizisubiri Arsenal, Crystal Palace
Muktasari:
- Manchester City ilitwaa taji hilo kwa mara ya nne mfululizo mwaka 2021, lakini haijafika nusu fainali tangu hapo. Newcastle, kwa upande wake, iliifunga Liverpool mwezi Machi 2025 na kutwaa kombe lao la kwanza la ndani baada ya kusubiri kwa miaka 70.
NEWCASTLE United itakabiliana na mabingwa mara nane wa Kombe la Carabao, Manchester City, katika hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo.
Katika nusu fainali nyingine itakayochezwa kwa mfumo wa mechi mbili (nyumbani na ugenini), Chelsea itakutana ama na Arsenal au Crystal Palace, ambapo italazimika kusubiri hadi Jumanne ijayo Desemba 23, 2025 ili kujua ni mpinzani gani kati ya wapinzani wao wa jijini London watakutana hatua hiyo.
Mechi ya robo fainali kati ya Arsenal na Crystal Palace ambayo awali ilitakiwa kuchezwa katikati ya wiki hii, imeahirishwa ili kuzuia timu ya Palace inayonolewa na Oliver Glasner kushuka dimbani mara tatu ndani ya siku tano, kutokana na ushiriki wao kwenye Europa Conference League. Leo Alhamisi itacheza dhidi ya Kuopion Palloseura.
Mechi za mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya Carabao zitachezwa katika wiki inayoanza Januari 12, 2026, huku marudiano ikipangwa kuchezwa katika wiki inayoanza Februari 2, 2026.
Chelsea ilimaliza kama washindi wa pili dhidi ya Liverpool katika fainali za mwaka 2022 na 2024. Mara ya mwisho ilishinda taji hilo mwaka 2015.
Manchester City ilitwaa taji hilo kwa mara ya nne mfululizo mwaka 2021, lakini haijafika nusu fainali tangu hapo. Newcastle, kwa upande wake, iliifunga Liverpool mwezi Machi 2025 na kutwaa kombe lao la kwanza la ndani baada ya kusubiri kwa miaka 70.
RATIBA KAMILI YA NUSU FAINALI
Chelsea vs Arsenal/Crystal Palace
Newcastle vs Manchester City