Neto aomba radhi kwa kumsukuma 'ball boy'
Muktasari:
- Tukio hilo lilitokea wakati Chelsea ilipokuwa inajaribu kusaka bao katika mchezo wa hatua ya 16 bora huku ikiwa nyuma kwa mabao 4-2.
PARIS, UFARANSA: WINGA wa Chelsea, Pedro Neto ameomba radhi hadharani baada ya kumsukuma muokota mipira ‘ball boy’ wakati wa mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya PSG katikati ya wiki hii.
Tukio hilo lilitokea wakati Chelsea ilipokuwa inajaribu kusaka bao katika mchezo wa hatua ya 16 bora huku ikiwa nyuma kwa mabao 4-2.
Neto alikuwa na haraka ya kuuchukua mpira ili kuanza mchezo upya, lakini katika harakati hizo alimgonga na kumsukuma ball boy ambaye alianguka hadi kwenye mabango ya matangazo. Kitendo hicho kilizua hasira kwa wachezaji wa PSG waliokuwa karibu na eneo hilo, lakini cha kushangaza Neto hakupata hata kadi ya njano kutoka kwa mwamuzi, ingawa anaweza kuchukuliwa hatua na UEFA ikiwa utafanyika uchunguzi.
Akizungumza na kituo cha TNT Sports baada ya mechi, Neto alisema tukio hilo lilitokea kutokana na presha ya mchezo.
“Nataka kumuomba radhi. Tayari nilizungumza naye. Ilikuwa ni katika joto la mchezo tu, damu ilishachemka. Tulikuwa tumeshaongozwa na nilitaka kuuchukua mpira haraka. Nilimsukuma kidogo na najua sikutakiwa kufanya vile,” alisema Neto baada ya kumalizika kwa mechi hiyo ambayo Chelsea ilipokea kichapo cha mabao 5-2.
Neto aliongeza kuwa mara baada ya tukio hilo alimfuata ball boy huyo na kumpa jezi yake kama ishara ya kuomba msamaha.
“Niligundua nimemuumiza na mimi si mtu wa aina hiyo. Nilimpa jezi yangu na kumuomba radhi mara nyingi sana. Nadhani nilisema samahani kama mara 35,” alisema.
Tukio hilo limewakumbusha mashabiki tukio la mwaka 2013 ambapo nyota wa zamani wa Chelsea Eden Hazard aligombana na ball boy wa Swansea City wakati wa nusu fainali ya EFL Cup.
Katika tukio hilo Hazard alimrukia ball boy kwa kumkanyaga ili kuupata mpira, kitendo kilichomfanya apewe kadi nyekundu na kufungiwa mechi tatu.