NDO HIVYO... RONALDO HAYUMO!

Thursday February 18 2021
ronaldo pic

LONDON, ENGLAND. HAWA jamaa wapo siriazi kweli? Ni Gary Neville na Jamie Carragher wametaja tano bora ya usajili wa muda wote kwenye Ligi Kuu England - na kubaki au kataa, Cristiano Ronaldo hayumo.

Mabeki hao wa zamani waliotamba na Manchester United na Liverpool mtawalia ambao kwa sasa ni wachambuzi wa soka kwenye televisheni ya Sky Sport, walitaja tano bora yao ya usajili wa muda wote kwenye Ligi Kuu England wakimweka kando Mreno Ronaldo, licha ya kuhesabika kuwa mmoja wa wachezaji bora kabisa waliowahi kutokea kwenye ligi hiyo.

Man United ilimsajili Ronaldo, 36, kutoka Sporting Lisbon kwa ada ya Pauni 17 milioni, Agosti 2003 na alitamba kwenye kikosi hicho sambamba na Neville kabla ya kuuzwa Real Madrid kwa ada iliyovunja rekodi ya dunia kwa wakati huo - Pauni 85 milioni mwaka 2009.

Ronaldo alifunga mabao 118 na kuasisti mara 69 katika mechi 292 alizoichezea Man United na alibeba tuzo ya Ballon d’Or akiwa na kikosi hicho kabla ya kutimkia Madrid, ambako alikwenda kuchuana jino kwa jino na Lionel Messi.

Huko Real Madrid alikwenda kuwa bora zaidi akifunga mabao 450 na kuasisti mara 132 katika mechi 438 huku akiongeza tuzo nne za Ballon d’Or na hivyo kumfanya awe amefikisha tuzo tano za ubora wa dunia.

Na sasa anakipiga kwenye kikosi cha Juventus alikofunga mabao 88 na kuasisti mara 21 katika mechi 115, hiyo ni kabla ya mechi ya usiku wa jana Jumatano kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya FC Porto.

Advertisement

Lakini, licha ya mchango wake mkubwa kwenye kikosi cha Man United ambapo alibeba mataji matatu ya Ligi Kuu England na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya, wachambuzi hao wa Sky wameshindwa kumuweka kwenye orodha ya usajili bora kabisa kuwahi kutokea kwenye Ligi Kuu England.

Chaguo la kwanza la wakongwe lilikuwa Alan Shearer aliyenaswa na Blackburn kutoka Southampton kwa ada ya Pauni 3.6 milioni mwaka 1992. Shearer ndiye kinara wa muda wote wa mabao kwenye Ligi Kuu England akifunga mara 260, huku akiweka rekodi ya kufunga mabao 34 katika msimu wa 1994-95 alipoisaidia Rovers kushinda ubingwa wa ligi.

Eric Cantona ametajwa pia kwenye orodha huyo kwa uhamisho wake wa kutoka Leeds United kwenda Man United kwa ada ya Pauni 1.2 milioni mwaka 1992. Staa huyo wa Ufaransa aliisaidia Man United kushinda mataji manne ya ligi, mwaka 1993, 1994, 1996 na 1997.

Gwiji wa Arsenal, Thierry Henry aliyenaswa kutoka Juventus kwa ada ya Pauni 10.5 milioni mwaka 1999 naye ameingia kwenye orodha hiyo, huku akiisaidia miamba hiyo ya Emirates kushinda mataji kadhaa ya Ligi Kuu England akicheza kwa msimu mzima bila ya kupoteza mechi kwenye ligi hiyo.

Beki Vincent Kompany na straika Jamie Vardy wanakamilisha tano bora ya wakongwe hao. Kompany alitua kwenye Ligi Kuu England akitokea Hamburg kwa ada ya Pauni 6.7 milioni mwaka 2008 na Vardy alisajiliwa na Leicester City kwa Pauni 1 milioni akitokea timu ya mchangani ya Fleetwood Town mwaka 2012.

Carragher alisema anamkubali zaidi Vardy kwa namna alivyo-tokea mchangani na kuja kuipa Leicester City ubingwa wa kihistoria kwenye Ligi Kuu England, akiamini huo ndio usajili bora kuliko wote wakati mwenzake, Neville anadhani usajili bora zaidi ni wa Cantona.

Pengine wakongwe hao walizingatia ada za uhamisho zilizolipwa kwa kipindi hicho, licha ya kwamba Ronaldo alikuwa moto uwanjani, lakini alinaswa kwa pesa nyingi - karibu Pauni 20 milioni. Hata hivyo, jambo hilo liliwagawa mashabiki kibao na kuweka maoni yao kwenye mitandao ya kijamii.

Shabiki mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Ashley aliandika: “Frank Lampard (kwenda Chelsea)… Pauni 14 milioni, Ligi Kuu mara tatu - Ligi ya Mabingwa Ulaya, Europa League, FA mara nne na Kombe la Ligi mara mbili. Mabao mengi zaidi kutokea kwenye kiungo - mabao 20+ kwa misimu mitano mfululizo...haelezeeki.”

Mwingine aliyefahamika kwa jina la Zizou aliongeza: “Sol Campbell hakika anapaswa kuingia...usajili wa bure kwa beki wa kiwango cha dunia.”

Na shabiki wa tatu, Sonny aliandika: “Namfikiria (Gianfranco) Zola pia, maana alibadili kabisa akili za watu wa Stamford Bridge.”

Advertisement