Ndinga za kifahari kwa mastaa NBA
Muktasari:
- Kutoka kuwa na Rolls-Royce hadi Lamborghini, mastaa wengi wa NBA wamegeuza barabara za mijimbo mbalimbali ya Marekani kuwa onyesho la uwezo walionao kifedha na hapo achana na mijengo mikali wanayomiliki.
TEXAS, MAREKANI: ‘WANATESA kote kote.’ Ndicho unaweza kusema kwa mastaa wa mpira wa kikapu huko Marekani kama vile LeBron James na Stephen Curry kutokana na magari ya kifahari wanayomiliki.
Kutoka kuwa na Rolls-Royce hadi Lamborghini, mastaa wengi wa NBA wamegeuza barabara za mijimbo mbalimbali ya Marekani kuwa onyesho la uwezo walionao kifedha na hapo achana na mijengo mikali wanayomiliki.
Leo tunakuletea wachezaji watano wa NBA wanaoongoza kwa umiliki wa magari ya kifahari pamoja na thamani halisi.
LEBRON JAMES (Rolls-Royce Cullinan)
Ni ngumu kuzungumzia NBA bila kutaja jina la LeBron James. King James amekuwa ishara ya mafanikio kwa zaidi ya miaka 20.
Nje ya uwanja, anapendelea vitu vya hadhi kubwa na miongoni mwa magari ya kifahari anayomiliki ni pamoja na Rolls-Royce Cullinan ambalo linatajwa kuwa na thamani ya Dolla 400,000 (zaidi ya Sh 1.04bilioni)
Rolls-Royce Cullinan ni gari la kifahari zaidi katika kundi la SUV, likiwa na injini yenye nguvu zaidi. Gari hili lina utulivu wa ajabu na mfumo wa ndani unakufanya mtumiaji kujisikia raha wakati ukiendesha ikiwemo kupasha viti joto ikiwa kuna baridi.
Mbali na Cullinan, LeBron pia anamiliki Ferrari F430 Spider, Lamborghini Aventador na Porsche 911 Turbo S.
STEPHEN CURRY (Porsche 911 GT3 RS)
Nahodha wa Golden State Warriors anaamini katika ‘ubora wa ukimya’, unajua kwa nini? Jamaa anapendelea magari yenye teknolojia na usahihi zaidi kuliko yale yenye makelele ya injini.
Gari lake pendwa ni Porsche 911 GT3 RS ambalo linatajwa kuwa na thamani ya dolla 223,800 (zaidi ya Sh582 milioni), moja ya magari ya michezo yenye mvuto sana.
Lina injini yenye nguvu na uwezo wa kufikia kasi ya 100 km/h ndani ya sekunde tatu. Gari hili lina mfumo maalum unaosaidia kwenye kuthibiti kasi kwa ajili ya usalama.
KEVIN DURANT (Ferrari California)
Kevin Durant ambaye amewahi kushinda mataji mawili ya NBA Finals MVP, anamiliki Ferrari California.
Ferrari California ina injini ya V8 yenye uwezo wa kufikia kasi ya 310 km/h.
Ndinga hiyo inatajwa kuwa na thamani ya Dolla 205,000 (sh 534 milioni)
RUSSELL WESTBROOK (Lamborghini Aventador)
Uvaaji wake unaendana kabisa na gari analomiliki Lamborghini Aventador ya kijani kibichi ambayo inatajwa kuwa na thamani ya dolla 400,000 (Sh 1.04 bilioni)
Lamborghini Aventador inauwezo wa kufikia 0–100 km/h ndani ya sekunde 2.9 pekee. Ni gari linalojulikana kwa muundo wake wa milango inayofunguka ju na kelele ya injini kila unapoanza safari.
LUKA DONCIC (Lamborghini Urus)
Kijana kutoka Slovenia, Luka Doncic, amekuwa moja ya sura mpya za NBA. Katika umri wa miaka 26, ameshajijengea utajiri mkubwa na jina kubwa kutokana na kipaji chake.
Gari lake pendwa ni Lamborghini Urus inayotajwa kuwa na thamani ya dolla 260,000 (sh 678 milioni). Urus ina injini ya V8 yenye nguvu na uwezo wa kufikia kasi ya 305 km/h.
Ndani ya gari hili, kuna mfumo wa burudani wenye skrini tatu, sauti ya ubora wa juu kutoka Bang & Olufsen na viti vinavyoweza kupashwa joto au kupozwa kulingana na mahitaji.