NBA All-Stars ni mwisho wa enzi?

LEBRON James, kwa mara nyingine tena alitibua rekodi yake tamu ya kuwa mchezaji wa kwanza kwenye historia ya ligi ya kikapu Marekani (NBA), kuchaguliwa na kucheza kwa misimu 19 mfululizo ya mchezo mkubwa na maarufu wa NBA All-Star.

Mchezo huo ambao huchezwa kila msimu, hususan mwezi Februari kabla ya kila timu kukamilisha ngwe ya mwisho ya mechi za ligi ndefu (regular season), na kuingia kwenye mechi za mchujo (play-in) kwa sasa na mechi za mtoano (playoffs).

Imekuwa kawaida sasa kwa LeBron, siku anayovunja au kuweka rekodi ya jambo mojawapo kwenye zile rekodi zilizokuwepo awali kwenye ligi hiyo, lazima apoteze mchezo husika aliocheza siku hiyo na kuweka rekodi.

Kuanzia rekodi ya karibuni ya ‘kuchumpa’ kuwa mchezaji wa nne kwa asisti nyingi zaidi kihistoria, alipofikisha asisti 10,336 lakini pia siku aliyovunja na kuweka rekodi ya ufungaji bora wa muda wote wa pointi 38,387 za Kareem Abdul-Jabbar zilizodumu kwa miaka 40.

Safari hii ni juzi Jumatatu asubuhi, LeBron alivunja rekodi ya Kareem tena kwa kuchaguliwa na kucheza mchezo wa All-star kwa mara ya 19 tena mfululizo, lakini hata hivyo alipoteza mchezo huo kwa timu yake kufungwa vikapu 184-175 na timu ya Giannis Antetokounmpo.


MSHANGAO WA MVP JOKIC

Mchezo huo unaohusisha wachezaji waliofanya vizuri kwenye ligi msimu huu, ulichezwa mjini Utah na kuna timu ya Utah Jazz iliyowakilishwa na mchezaji Lauri Markannen aliyechaguliwa wa mwisho kwenye ‘draft’ ya wachezaji wa kuanza (starter).

Nahodha wa Magharibi, LeBron James alikuwa wa kwanza kuchagua wa kuanza wakati Giannis wa Mashariki alianza kuchagua wale wa akiba.

Kivutio kikubwa ni MVP mara mbili wa ligi hiyo Nikola Jokic ‘kupotezewa’ na manahodha wote wawili hadi walipobaki wawili naye akijua kabaki mwenyewe, Nikola alijipeleka kwa LeBron bila kuitwa, kabla ya baadaye kukiri hakujua kama walibaki wawili yeye na Markannen aliyeenda kwa Giannis.


REKODI POINTI MVP TATUM

Lengo la pointi kwenye mchezo huo ilikuwa ni timu itakayofikisha pointi 184 au zaidi, kama ilivyozoeleka kwenye misimu ya karibuni, mara zote timu ya LeBron ndiye hufikia idadi husika ila safari hii, Jayson Tatum aliongoza maangamizi kwa kufunga pointi 55.

Mara ya mwisho Anthony Davis ndiye aliweka rekodi ya kufunga pointi 52 mwaka 2017, huku Damian Lillard kwa msimu wa pili mfululizo alifunga tena pointi tatu za mwisho kumaliza mchezo, msimu jana alifanya hivyo akiwa timu ya LeBron, safari hii amefanya akiwa timu ya Giannis.


MUUNDO MPYA NI SHIDA

Kwa msimu wa sita sasa, shirikisho chini ya kamishna Adam Silver, lilibadilisha mfumo wa kuchezwa kwa mchezo huo na mwaka 2017 kurudi nyuma, ulitumika muundo wa timu ya Ukanda wa Mashariki dhidi ya Magharibi, lakini kutokana na Magharibi kushinda mfululizo, wakaamua kubadilisha ili kuongeza msisimko.

Ndani ya mabadiliko hayo, ndipo ikawa kila ukanda unaongozwa na manahodha ambao wanakuwa wamepigiwa kura nyingi zaidi na mashabiki, vyombo vya habari na wachezaji wenyewe. Hata hivyo, muundo huo sasa umeshachokwa nao baada ya kusisimua kwenye misimu miwili hadi mitatu ya mwanzo lakini kuanzia msimu wa nne hadi sasa wa sita, umepondwa.

Mashabiki wengi na wadau wa ligi hiyo wameonyesha kuuchoka mfumo huo na wameendelea kuandika kwenye kurasa rasmi za mitandao ya ligi hiyo, wakipendekeza mfumo ubadilishwe tena wengi wao wakitamani urudishwe muundo wa zamani wa kuhusisha mastaa wa kila ukanda ili kunogesha ushindani wa kanda na sio wachezaji.

Ukosoaji mwingine umeelekezwa kwa wachezaji wengi kucheza mchezo huo kwa hofu ya kutokuumia ili kucheza mechi za mchujo au mtoano kwa timu zao.

Swali linabaki, shirikisho litasikiliza maoni ya mashabiki na wadau kwa kurudisha muundo wa zamani au kuubadili upya kwa msimu ujao ambao utachezwa mjini Indianapolis.