Nahodha Super Falcons asikitishwa kuahirishwa kwa WAFCON 2026
Muktasari:
- Mashindano hayo, ambayo awali yalipangwa kuanza Machi 17, 2026 nchini Morocco, yameahirishwa na sasa yataanza Julai 25, 2206 hadi Agosti 16, 2026. CAF ilitoa taarifa hiyo jana Alhamisi, ikitaja changamoto ambazo hazikutarajiwa kama sababu ya mabadiliko hayo ya ghafla.
NAHODHA wa timu ya taifa ya wanawake ya Nigeria maarufu Super Falcons, Rasheedat Ajibade, ameeleza kusikitishwa kwake na uamuzi wa ghafla wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) wa kusogeza mbele tarehe za kuanza kwa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON 2026).
Mashindano hayo, ambayo awali yalipangwa kuanza Machi 17, 2026 nchini Morocco, yameahirishwa na sasa yataanza Julai 25, 2206 hadi Agosti 16, 2026. CAF ilitoa taarifa hiyo jana Alhamisi, ikitaja changamoto ambazo hazikutarajiwa kama sababu ya mabadiliko hayo ya ghafla.
Ajibade, ambaye ni mmoja wa nyota wakubwa wa soka la wanawake barani Afrika, ametumia ukurasa wake mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter) kuonyesha kutoipokea vyema taarifa hiyo. Katika ujumbe wake mfupi lakini wenye uzito, akiandika: "Soka la wanawake barani Afrika linastahili ubora zaidi," akisindikiza ujumbe huo na emoji inayoonyesha masikitiko makubwa.
Uamuzi huu umekuja wakati timu nyingi zikiwa katika hatua ya mwisho ya maandalizi. Kwa mfano, Super Falcons ilikuwa imetoka kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Cameroon wiki iliyopita kama sehemu ya kujiweka sawa kwa ajili ya safari ya kuelekea Morocco mwezi huu wa Machi.
Kusogezwa huku kwa mashindano kumezua mjadala mpana miongoni mwa wadau wa soka, wengi wakihoji umakini wa CAF katika kuratibu mashindano ya wanawake ikilinganishwa na yale ya wanaume.