Mwendo wa kutafutana UEFA!
Muktasari:
- Arsenal ina rekodi ya asilimia 100 ya ushindi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu huku ikifunga mabao 14 na kufungwa moja tu, ikiandikisha takwimu safi kabisa za mabao +13.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL inashika usukani katika mchakamchaka wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye hatua ya makundi inayochezwa kwa mfumo wa ligi baada ya kukusanya pointi 15 katika mechi tano ilizocheza.
Arsenal ina rekodi ya asilimia 100 ya ushindi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu huku ikifunga mabao 14 na kufungwa moja tu, ikiandikisha takwimu safi kabisa za mabao +13.
Kipute hicho cha Ligi ya Mabingwa Ulaya kinaendelea Jumanne hii, kwa kushuhudia mechi kibao, ikiwamo ile ya Inter Milan kumenyana na Liverpool uwanjani San Siro. Mechi hiyo inasubiriwa kwa hamu kuona kama kuna kitu kipya inaweza kufanya Liverpool kutokana na matokeo yao ya siku za karibuni kutokuwa yakuridhisha.
Hata hivyo, kutakuwa na mechi ya mapema kabisa, ambapo Kairat Almaty itakipiga na Olympiacos, wakati Bayern Munich itakuwa na kasheshe zito uwanjani Allianz Arena kwa kukipiga na Sporting CP.
AS Monaco itaulizana maswali na Galatasaray, huku Waitaliano Atalanta wakiwa na shughuli pevu ya kuikabili Chelsea, wakati Barcelona itakuwa nyumbani kucheza na Eintracht Frankfurt ya Ujerumani. Ukiweka kando mechi hizo, kutakuwa na mchakamchaka wa mechi nyingine kwa Jumanne hii, ambapo PSV Eindhoven itakipiga na Atletico Madrid, wakati Tottenham Hotspur itamaliza utata na Slavia Prague huku Union St Gilloise itakuwa nyumbani kucheza na Marseille ya Ufaransa katika moja ya mechi zenye ushindani mkali.
Kasheshe litaendelea Jumatano, ambapo mechi inayosubiriwa kwa hamu zaidi ni ile ya Bernabeu, ambapo Real Madrid itakuwa nyumbani kukabiliana na Manchester City.
Real Madrid ya kocha Xabi Alonso imekuwa na matokeo yanayozua maswali kwa siku za karibuni, hivyo kipute hicho cha kuikabili Man City kinaweza kuwa mtihani mzito kwa kocha huyo Mhispaniola, ambaye atakabiliana na Mhispaniola mwenzake, Pep Guardiola.
Vinara Arsenal watakuwa ugenini kukabiliana na Club Brugge, wakati ambao kocha Mikel Arteta atataka kukirudisha kikosi chake kwenye njia za ushindi baada ya kukumbana na kipigo kwenye mechi iliyopita kwenye Ligi Kuu England ilipotandikwa 2-1 na Aston Villa.
Mechi nyingine za kibabe zitashuhudiwa wakati Qarabag FK itakapocheza na Ajax, Villarreal na FC Copenhagen, huku Athletic Bilbao ikicheza na mabingwa watetezi, Paris Saint-Germain.
Bayer Leverkusen itakuwa nyumbani Ujerumani kukabiliana na Newcastle United, huku Benfica ikikipa na Napoli, Borussia Dortmund na Bodoe/Glimt na Juventus itamaliza ubishi na Pafos FC katika mechi itakayofanyika huko Italia. Itakuwaje?