Musiala amkosesha raha Donnarumma

Muktasari:
- Kipa huyo alikuwa golini kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la Dunia la Klabu dhidi ya Bayern Munich, ndipo lilipotokea tukio la kugongana na Musiala na mchezaji huyo kuvunja mguu wake.
MIAMI, MAREKANI: KIPA namba moja wa Paris Saint-Germain, Gianluigi Donnarumma ameangukia kilio uwanjani baada ya kuumizwa na kitendo cha kuhusika kwenye tukio la kuvunjika mguu Jamal Musiala.
Kipa huyo alikuwa golini kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la Dunia la Klabu dhidi ya Bayern Munich, ndipo lilipotokea tukio la kugongana na Musiala na mchezaji huyo kuvunja mguu wake.
Kwenye tukio la kugombea mpira, Musiala wakati akipambana na Willian Pacho, alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kipa Donnarumma kurukia mpira na kumlalia miguu na kumvunja.
Musiala alipiga kelele kali kutokana na maumivu na mguu wake ulionekana umepinda kwenye eneo la kifungo, kitu ambacho kiliwaumiza wachezaji wenzake walipokuwa wakiangalia mguu wa mwenzao huyo mwenye umri wa miaka 22.

Straika, Harry Kane alionekana akishika mikono kichwani kabla ya kuonyesha ishara ya machela iletwe uwanjani mapema. Kipa Donnarumma alionekana kuumizwa sana kwa tukio hilo na hivyo kuhitaji kutulizwa na makocha wake baada ya kuonekana kuwa kwenye hali ngumu.
Kipa huyo Mtaliano alinaswa na kamera za uwanjani akipiga goti moja kabla ya filimbi ya mapumziko na kuamua kuangua kilio.
Musiala alitolewa uwanjani kwa machela na kisha kupelekwa hospitali.
Kwa mujibu wa Sky Sports ya Ujerumani, winga huyo anaripotiwa kuvunjika mfupa wa fibula.
Kipa wa Bayern Munich, Manuel Neuer alimshushia lawama Donnarumma akisema: “Kwenye tukio kama lile huwezi kurukia mpira vile. Ile ilikuwa hatari. Alikuwa amejiandaa kumuumiza mwenzake.”
Baada ya mechi, Donnarumma aliposti picha yake inayomwonyesha akitokwa na machozi kwenye ukutasa wa Instagram na kuandika kuhusu Musiala, alisema: “Dua zangu zote na salamu za heri zikufikie @jamalmusiala10.”