Murillo atajwa Man United
Muktasari:
- Murillo ambaye ni miongoni mwa mastaa tegemeo wa Nottingham Forest hii sio mara yake ya kwanza kuwaniwa na vigogo wa England, aliwahi kuhusishwa na timu kubwa kadhaa katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana, lakini Forest iligoma kumuuza.
MANCHESTER United imeongeza jina la beki wa kimataifa wa Brazil, Murillo Santiago Costa dos Santos, 23, kwenye orodha ya wachezaji inaopambana kuwasajili katika dirisha lijalo la usajili la majira ya kiangazi.
Murillo ambaye ni miongoni mwa mastaa tegemeo wa Nottingham Forest hii sio mara yake ya kwanza kuwaniwa na vigogo wa England, aliwahi kuhusishwa na timu kubwa kadhaa katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana, lakini Forest iligoma kumuuza.
Manchester United inataka kuimarisha safu ya ulinzi kwa kuongeza beki kijana mwenye nguvu na pia inapitia wakati mgumu katika safu ya ulinzi ambapo licha ya kiwango bora cha Lisandro Martinez amekuwa nje kwa muda mwingi kutokana na majeraha ya mara kwa mara yanayomwandama.
Vilevile kwa sasa timu hiyo inamkosa Matthijs de Ligt ambaye naye pia amekuwa na panda shuka nyingi za majeraha ya mara kwa mara.
Mkataba wa sasa wa Murillo unatarajiwa kumalizika 2029 na tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 30 za michuano yote.
Mabosi wa Forest wanaweza kuhitaji zaidi ya Pauni 60 milioni ili kumuuza mchezaji huyo ikiwa yeye mwenyewe ataomba kuondoka.
Hata hivyo, pamoja na Man United, pia kuna timu kibao kutoka katika ligi tano bora za Ulaya ambazo zinamtaka.
Axel Disasi
WEST Ham United inapanga kumsainisha mkataba wa moja kwa moja beki wa kimataifa wa Ufaransa, Axel Disasi, 28, ikiwa timu hiyo itafanikiwa kubaki katika Ligi Kuu England. Disasi kwa sasa yupo West Ham kwa mkopo akitokea Chelsea, na kiwango chake kimewashawishi mabosi kufikiria kumbakisha. Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa West Ham haitakuwa tayari kulipa kiasi cha Pauni 38.8 ambacho Chelsea ilitoa 2023 ili kumsajili beki huyo.
Tino Livramento
ARSENAL inafikiria kuwasilisha ofa ya kumsajili beki wa kulia wa Newcastle United na timu ya taifa ya England, Tino Livramento, 23, katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi. Taarifa zinaeleza Arsenal inaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya mkataba wa beki huyo ambao kwa sasa unatarajiwa kumalizika 2028. Livramento bado hajaonyesha dalili za kutaka kuongeza mkataba mpya na Newcastle, jambo linaloifanya Arsenal kuamini inaweza kumpata kirahisi.
Julian Brandt
ASTON Villa imeingia katika vita dhidi ya Arsenal kwa ajili ya kuwania saini ya kiungo wa kimataifa wa Ujerumani, Julian Brandt, 29, anayekipiga Borussia Dortmund. Inaelezwa kuwa Villa inaamini itakutana na ushindani mkali kutoka kwa Arsenal, lakini imepanga kutoa ofa nono ili kuhakikisha inashinda na inaipata huduma yake. Brandt anatarajiwa kuwa mchezaji huru mwishoni mwa msimu huu.
Marcos Senesi
JUVENTUS ipo tayari kuongeza juhudi zake katika vita ya kuiwania saini ya kumsajili beki wa kimataifa wa Argentina, Marcos Senesi, 28, anayekipiga Bournemouth. Mabosi wa Juventus wamekuwa katika mazungumzo na wawakilishi wa nyota huyo na wana matumaini makubwa ya kumsajili staa huyo ambaye mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu. Senesi amekuwa miongoni mwa mabeki muhimu wa Bournemouth.
Felix Nmecha
KIUNGO wa kimataifa wa Ujerumani, Felix Nmecha, 25, anatarajiwa kusaini mkataba mpya wa muda mrefu na Borussia Dortmund utakaomuweka katika kikosi hicho hadi 2030. Taarifa zinaeleza Dortmund imefikia hatua nzuri ya makubaliano na kiungo huyo ili kuhakikisha anaendelea kuwa sehemu muhimu ya kikosi hicho kwa miaka mingi ijayo. Hatua hiyo inatajwa kuwa ni mkakati wa klabu hiyo kumbakiza nyota huyo.
Finn Jeltsch
LIVERPOOL na Arsenal zinaongoza katika mbio za kumsajili beki kijana wa VfB Stuttgart na timu ya taifa ya Ujerumani chini ya miaka 21, Finn Jeltsch, 19. Inaelezwa kuwa klabu zote mbili zimekuwa zikifuatilia kwa karibu maendeleo ya beki huyo chipukizi na maskauti wamekuwa wakimtazama kwa karibu zaidi. Hata hivyo, hazipo zenyewe katika mbio hizo kwani Bayern Munich pia imeonyesha nia juu yake.
Joshua Zirkzee
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uholanzi, Joshua Zirkzee, 24, anadaiwa kutaka kuondoka Manchester United katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi. Taarifa zinaeleza kuwa mshambuliaji huyo alitaka kuondoka hata katika dirisha la usajili la Januari, lakini Man United ilizuia mpango huo. Licha ya kushindwa wakati huo, taarifa zinadai Zirkzee ana nia ya kuondoka ili kutafuta changamoto mpya.